>Mwanzo >Masomo >Kukabiriana na kumbukumbu ya maisha yetu

Kukabiriana na kumbukumbu ya maisha yetu

KUKABILIANA NA KUMBUKUMBU YA MAISHA YETU

 "Kazi ya kila mtu inachunguzwa mbele za Mungu na inaandikwa kama ni ya UAMINIFU ama ya KUKOSA UAMINIFU. Mbele yake kila jina katika vitabu vya mbinguni huandikwa kwa usahihi kabisa kila neno baya, kila tendo la uchoyo [ubinafsi], kila kazi isiyotimizwa, na kila dhambi ya siri, na kila unafiki uliofanywa kwa werevu. Maonyo yaliyotumwa kutoka mbinguni na makaripio YALIYOPUUZWA, wakati uliopotezwa bure [kucheza karata, bao, n.k.], nafasi ambazo hazikutumiwa vizuri, mvuto uliotolewa kwa WEMA au kwa UBAYA, pamoja na matokeo yake yafikayo mbali, vyote hivi vinawekwa katika kumbukumbu zenye tarehe na malaika yule anayetunza kumbukumbu hizo.

Kipimo kitakachotumika katika hukumu.

 SHERIA YA MUNGU [AMRI KUMI] ndicho KIPIMO ambacho kwacho TABIA na MAISHA ya wanadamu vitapimwa katika hukumu hii [inayoendelea mbinguni sasa]. Asema yule mwenye hekima: "Mche Mungu, nawe UZISHIKE AMRI ZAKE [KUMI]. Maana kwa jumla ndiyo IMPASAYO [WAJIBU WAKE] mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila KAZI, pamoja na kila NENO LA SIRI, likiwa JEMA au likiwa BAYA." Mhubiri 12:13,14. Mtume Yakobo anawaonya ndugu zake:  "SEMENI ninyi, na KUTENDA kama watu WATAKAOHUKUMIWA KWA SHERIA YA UHURU [AMRI KUMI]. Yakobo 2:12.

 Wale ambao katika hukumu hii wana"hesabiwa kuwa  wamestahili" watakuwa na sehemu yao katika UFUFUO WA WENYE HAKI. Yesu alisema: "Wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kufufuka katika wafu... huwa sawasawa na malaika; nao ni wana [watoto] wa Mungu, kwa vile walivyo wana [watoto] wa ufufuo." Luka 20:35,36. Tena anatangaza kwamba "wale waliofanya mema" watatoka "kwa UFUFUO WA UZIMA." Yohana 5:29. Wenye haki waliokufa [hawako mbinguni] hawatafufuliwa mpaka baada ya HUKUMU HII KUFUNGWA ambayo kwayo WATAHESABIWA kuwa wamestahili kuupata "ufufuo wa uzima." Tangu SASA wao hawatahudhuria KIMWILI katika MAHAKAMA [ile mbinguni] wakati KUMBUKUMBU zao zinapochunguzwa na KESI zao KUKATWA. [2 Wakorintho 5:l0].

 Yesu atatokea pale kama MTETEZI [MWOMBEZI] wao, kuwaombea mbele zake Mungu. "Na kama mtu akitenda dhambi tunaye MWOMBEZI [MTETEZI] kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki." l Yohana 2:1.  "Kwa sababu Kristo hakuingia PATAKATIFU palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa PATAKATIFU HALISI; bali aliingia MBINGUNI HASA, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu." "Naye, kwa sababu hii, aweza KUWAOKOA KABISA wao wamjiao Mungu kwa Yeye;  maana YU HAI sikuzote ili AWAOMBEE." Waebrania 9:24; 7:25.

 Kumbukumbu (Vitabu) Kufunuliwa

 Vitabu vya kumbukumbu vinapofunuliwa katika hukumu hii, MAISHA ya wale wote WALIOPATA KUMWAMINI YESU yanachunguzwa mbele zake Mungu [bila wao kuwapo kimwili]. Kuanzia na wale waliotangulia kuishi kwanza duniani humu [Adamu na Hawa], Mtetezi wetu anazishughulikia KESI za kila kizazi kilichofuata zinazotajwa mbele Yake, na kufunga na [kesi za] walio hai [sasa]. Kila jina linatajwa, kila kesi inachunguzwa kwa makini sana. Majina YANAKUBALIWA, majina YANAKATALIWA. Wakati  atakapokuta watu wo wote wanazo dhambi zilizobaki katika vitabu vile vya kumbukumbu, ambazo HAZIJATUBIWA wala KUSAMEHEWA,  majina yao YATAFUTWA katika kitabu cha uzima, na kumbukumbu ya MATENDO YAO MEMA itafutwa katika KITABU CHA UKUMBUSHO cha Mungu. Mungu alimtangazia Musa: "BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote ALIYENITENDA DHAMBI ndiye NITAKAYEMFUTA katika kitabu changu." Kutoka 32:33. Naye nabii Ezekieli asema: "Bali  MWENYE HAKI atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na KUTENDA UOVU ... Katika MATENDO yake yote ya HAKI aliyoyatenda HALITAKUMBUKWA hata mojawapo." Ezekieli 18:24.

 Wale waliotubu dhambi zao kweli kweli, na kwa imani kudai damu yake Kristo kama kafara ya upatanisho wao, mbele ya majina yao katika vitabu vya mbinguni umeandikwa MSAMAHA; wamekuwa washirika wa HAKI yake Kristo, na TABIA zao zimeonekana kuwa zinapatana kabisa na Sheria ya Mungu [Amri Kumi], DHAMBI zao ZITAFUTWA, na wenyewe watahesabiwa kuwa wanastahili kuupata UZIMA WA MILELE. Kupitia kwa nabii Isaya, Bwana anatangaza hivi: "Mimi, naam, Mimi, ndimi NIYAFUTAYE makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala SITAZIKUMBUKA dhambi zako." Isaya 43:25. Alisema Yesu: "Yeye ASHINDAYE [DHAMBI] atavikwa hivyo MAVAZI MEUPE [HAKI YA KRISTO], wala SITALIFUTA kamwe JINA LAKE  katika KITABU CHA UZIMA, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake." "Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni."  Ufunuo 3:5; Mathayo 10:32,33.

 Mwombezi wetu wa kimbingu anatoa ombi kwamba wale wote walioshinda kwa njia ya imani katika damu Yake WASAMEHEWE dhambi zao, kwamba wapate KUREJESHWA KWENYE MAKAO YAO YA EDENI, na KUVIKWA TAJI kama WARITHI pamoja naye wa ile "MAMLAKA YA KWANZA" [aliyoipoteza Adamu]. Mika 4:8. Shetani katika juhudi yake yote ya KULIDANGANYA na KULIJARIBU taifa letu [la kibinadamu] alikuwa amefikiria KUUVURUGA mpango wa Mungu wa kumwumba mwanadamu; walakini Kristo SASA anamwomba [Baba Yake] kwamba MPANGO HUO SASA UTEKELEZWE kana kwamba MWANADAMU alikuwa HAJAPATA KUANGUKA [DHAMBINI] KAMWE. Anawaombea watu Wake sio tu MSAMAHA na KUHESABIWA HAKI kikamilifu kabisa, bali kwamba WAPATE KUSHIRIKI katika UTUKUFU Wake na KUKETI katika KITI CHAKE cha Enzi.

Kuzifuta dhambi

 Kazi ya HUKUMU YA UPELELEZI (INVESTIGATIVE JUDGMENT) na  KUZIFUTA DHAMBI (THE BLOTTING OF SINS) itakwisha KABLA ya marejeo ya pili ya Bwana [wetu]. Kwa vile wafu wanapaswa kuhukumiwa kutokana na mambo yaliyoandikwa katika vitabu vile, haiwezekani kabisa kwamba dhambi za wanadamu zifutwe isipokuwa mpaka BAADA ya [kufungwa] hukumu hiyo ambayo kwayo KESI zao zinapaswa kuchunguzwa. Walakini Mtume Petro anaeleza wazi ya kwamba dhambi za WAUMINI zitafutwa zitakapokuja "nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo."  Matendo Mitume 3:19,20. Hukumu ya Upelelezi itakapofungwa, KRISTO ATAKUJA, na UJIRA [MSHAHARA] Wake utakuwa pamoja naye KUMLIPA KILA MTU KAMA KAZI [MATENDO] YAKE ILIVYO. [Ufunuo 22:l2; Warumi 6:23].

 Katika huduma ile ya PATAKATIFU PA DUNIANI, Kuhani Mkuu, baada ya kufanya UPATANISHO kwa ajili ya Israeli, alitoka nje na KUWABARIKI mkutano. Hivyo ndivyo Kristo naye, mwisho wa kazi yake kama MPATANISHI, atatokea, 'pasipo dhambi, kwa HAO WAMTAZAMIAO KWA WOKOVU,' (Waebrania 9:28), na KUWABARIKI watu Wake wanaomngojea kwa kuwapa UZIMA WA MILELE. Kama vile yule Kuhani katika kuiondoa dhambi kutoka katika PATAKATIFU,  alivyoziungama dhambi juu ya kichwa cha Mbuzi wa Azazeli, hivyo ndivyo naye Kristo atakavyoweka dhambi zote hizo juu ya SHETANI, Mwasisi na Mchochezi wa dhambi zote. Yule Mbuzi wa Azazeli, akiwa amebeba dhambi za Israeli, alipelekwa mbali katika nchi  "ISIYO NA WATU" (Mambo ya Walawi 16:22); hivyo ndivyo naye SHETANI, akiwa amechukua HATIA YA DHAMBI ZOTE alizowasababisha watu wa Mungu kuzitenda, atafungwa kwa MIAKA ELFU MOJA humu duniani, ambayo kwa wakati huo ITAKUWA UKIWA [TUPU], HAINA WATU, na hatimaye atapata adhabu kamili ya dhambi zake katika MOTO ule utakaowaangamiza waovu wote. [Ufunuo 20:9,10,15;  Malaki 4:1-3; Ezekieli 28:l4,l5,l7-l9]. Hivyo ndivyo MPANGO ULE MKUU WA UKOMBOZI utakavyofikia UTIMILIFU wake katika tendo la mwisho la KUFUTILIA MBALI DHAMBI na KUWAKOMBOA wale wote waliopenda KUACHANA NA UOVU WOTE.

Njia ya Utakatifu

 Wale watakaoshiriki manufaa ya kazi ya Mwokozi ya UOMBEZI [UPATANISHO] wasiruhusu kitu cho chote kuingilia kati hilo JUKUMU lao la KUKAMILISHA UTAKATIFU katika kicho chake Mungu.  Saa zao za thamani, badala ya kuzitumia kwa mambo ya ANASA, KUJIONYESHA, au KUTAFUTA FAIDA, wangezitumia kwa KUJIFUNZA NENO LA KWELI kwa bidii na maombi. Somo la PATAKATIFU (THE SANCTUARY) na HUKUMU YA UPELELEZI (THE INVESTIGATIVE JUDGMENT)  yanapaswa kueleweka kwa WAZI na watu Wake Mungu. Wote wanahitaji KUJUA wao wenyewe MAHALI ALIPO NA KAZI ANAYOFANYA  Kuhani wao Mkuu [Yesu Kristo]. La sivyo, itakuwa HAIWEZEKANI kwao kuitumia imani yao ambayo ni ya muhimu kwa WAKATI HUU au KUKALIA NAFASI ambayo Mungu amekusudia waijaze. Kila mtu mmoja mmoja anayo roho yake ya KUIOKOA au KUIPOTEZA. Kila mmoja ana KESI [Kuna Wakristo wanaodhani hawatahukumiwa ati kwa sababu wanamwamini Kristo] INAYOMNGOJEA katika MAHAKAMA ya Mungu [mbinguni]. Kila mmoja atakutana na JAJI MKUU ana kwa ana [kwa njia ya kumbukumbu katika vitabu --- 2 Wakorintho 5:10].  Basi, ni jambo la muhimu jinsi gani kwamba kila moyo [mtu] utafakari sana mara kwa mara mandhari ile ya kutisha wakati hukumu itakapowekwa na vitabu vitakapofunuliwa, wakati ule, pamoja na Danieli, kila mtu mmoja mmoja atasimama katika KURA [NAFASI] yake, mwisho wa siku zile. [Danieli 7:9,10; l2:13].

 Wale wote waliopata mwanga juu ya masomo haya [Patakatifu na Hukumu ya Upelelezi] wanatakiwa kutoa ushuhuda wao wa KWELI HIZI KUU ambazo Mungu amewakabidhi. PATAKATIFU PA MBINGUNI [HEKALU --- Ufunuo 11:19] ndicho KITOVU hasa cha KAZI YAKE KRISTO kwa niaba ya wanadamu. [Patakatifu hapo] PANAMHUSU kila mtu [roho] anayeishi duniani humu. Panatuonyesha sisi MPANGO WA UKOMBOZI, hadi mwisho kabisa wa wakati na kutufunulia suala lile la USHINDI MKUU WA PAMBANO kati ya HAKI na DHAMBI.  Ni jambo la muhimu sana kwamba WOTE wangeyachunguza MASOMO haya [mawili yaliyotajwa juu] kwa ukamilifu na kuweza kutoa jibu kwa kila mmoja anayewauliza sababu ya TUMAINI lililo ndani yao.

 Maombezi yake Kristo

 MAOMBEZI Yake Kristo kwa niaba ya mwanadamu katika PATAKATIFU PA MBINGUNI huko juu NI YA MUHIMU katika MPANGO WA WOKOVU kama kilivyokuwa KIFO CHAKE JUU YA MSALABA. Kwa njia ya KIFO Chake aliianza kazi ile ambayo baada ya ufufuo Wake alipaa mbinguni kwenda KUIKAMILISHA. KWA IMANI tunapaswa kuingia ndani ya PAZIA, "alimoingia Yesu kwa ajili yetu, MTANGULIZI wetu." Waebrania 6:20. Pale ndipo NURU itokayo katika MSALABA ule wa Kalvari INAAKISIWA (reflected). Pale ndipo tunapoweza kuelewa wazi SIRI ZA UKOMBOZI. WOKOVU wa mwanadamu unatimizwa kwa gharama KUBWA MNO kwa Mbingu; KAFARA  iliyotolewa ni sawa na madai ya SHERIA YA MUNGU ILIYOVUNJWA.  Yesu amefungua njia ya kwenda kwenye KITI CHA ENZI cha Baba, na kwa njia ya MAOMBEZI Yake shauku ya dhati ya wale wanaokuja Kwake kwa imani inaweza kufikishwa mbele zake Mungu.

 "Afichaye dhambi zake HATAFANIKIWA; bali yeye AZIUNGAMAYE na KUZIACHA atapata REHEMA." Mithali 28:13. Kama wale wanaoficha na kutoa udhuru kwa makosa yao WANGEWEZA KUONA jinsi Shetani ANAVYOWASIMANGA, na jinsi ANAVYOMDHIHAKI Kristo pamoja na Malaika Watakatifu kwa mwenendo wao [mbaya], wangefanya haraka KUUNGAMA dhambi zao na KUZIACHA. Kwa njia ya KASORO zilizo katika TABIA zetu, Shetani anafanya kazi ili KUUTAWALA MOYO WOTE, naye anajua kwamba kasoro hizo zikitunzwa [nasi], basi, ATAFANIKIWA [KUTUSHINDA]. Kwa hiyo, DAIMA anatafuta kuwadanganya wafuasi wake Kristo, akitumia HILA zake za kufisha ambazo haiwezekani kwao kuzishinda. Lakini Yesu ANAWAOMBEA akidai mikono Yake iliyojeruhiwa, na mwili Wake uliochubuliwa;  naye anawatangazia hivi wale wote ambao wangetaka kumfuata  "NEEMA YANGU YAKUTOSHA." 2 Wakorintho 12:9. "Jitieni NIRA yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni MPOLE na MNYENYEKEVU  wa moyo; nanyi mtapata RAHA nafsini mwenu. Kwa maana NIRA  Yangu [Amri Kumi] ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."  Mathayo 11:29,30. Hebu asiwepo hata mmoja anayedhani kwamba KASORO zake haziwezi KUPONYEKA. Mungu atatoa IMANI na NEEMA  ya kumwezesha KUSHINDA.

 HIVI SASA tunaishi katika SIKU KUU ILE YA UPATANISHO [au HUKUMU]. Katika huduma ya PATAKATIFU PA DUNIANI, Kuhani Mkuu alipokuwa anafanya UPATANISHO kwa ajili ya Israeli, WOTE WALITAKIWA KUJITESA NAFSI ZAO kwa KUTUBU dhambi zao na KUJINYENYEKEZA mbele zake Bwana, ili WASIJE WAKAKATILIWA MBALI [WAKAUAWA GHAFULA] na [kutengwa] na watu Wake. Kwa njia iyo hiyo, wale wote WANAOTAKA MAJINA YAO KUBAKI katika KITABU CHA UZIMA, wakati wamebakiwa na siku chache tu za MUDA WAO WA MAJARIBIO (PROBATION) [MATAZAMIO], wangejitesa nafsi zao SASA  mbele zake Mungu kwa KUHUZUNIKA [KUTUBU] kwa ajili ya dhambi zao na kuwa na TOBA YA KWELI. Lazima pawe na KUJICHUNGUZA SANA MOYO kwa uaminifu. Moyo ule wa kuyachukulia mambo haya kirahisi-rahisi tu na kimchezo hauna budi kuwekwa mbali. Kuna vita vinavyohitaji juhudi ambavyo viko mbele ya wote watakaotaka kushinda MIELEKEO YAO MIOVU ambayo inajitahidi  KUWATAWALA. Kazi ya KUJIWEKA TAYARI ni kazi ya kila mtu mmoja mmoja. HATUOKOLEWI KATIKA MAKUNDI. Usafi [wa maisha] na uchaji Mungu wa [mtu] mmoja HAUTAFIDIA upungufu wa SIFA hizo ndani ya [mtu] mwingine. Japokuwa mataifa yote yatapita katika  hukumu hii mbele zake Mungu, bado Yeye ATAICHUNGUZA KESI ya kila mtu mmoja mmoja kwa MAKINI SANA kana kwamba hapakuwa na kiumbe [mwanadamu] mwingine ye yote duniani. Kila mmoja hana budi kupimwa na kuonekana kuwa hana WAA wala KUNYANZI wala kitu cho chote kama hicho.

 Yanatisha mno matukio yale yahusikanayo na KUFUNGWA KWA KAZI YA UPATANISHO [mbinguni]. Ni ya maana kubwa sana mambo yaliyoko kule. HUKUMU INAENDELEA SASA KATIKA PATAKATIFU PA MBINGUNI. Kwa miaka mingi [tangu 1844] kazi hii imekuwa ikiendelea. UPESI ----- hakuna ajuaye ni upesi jinsi gani  ----- HUKUMU HIYO ITAWAFIKIA WALIO HAI [wanaoishi duniani sasa]. Katika hali ya kutisha sana mbele zake Mungu MAISHA yetu yataletwa KUCHUNGUZWA [sisi tutahukumiwa tukiwa hatuko kule kimwili -- Judgment in absentia]. Katika wakati huu kuliko wakati mwingine wo wote inampasa KILA MTU kusikia ONYO hili la Mwokozi, "Angalieni, KESHENI [Ombeni], kwa kuwa HAMJUI wakati ule utakapokuwapo." Marko 13:33. "Walakini USIPOKESHA,  nitakuja kama mwivi, wala HUTAIJUA saa nitakayokuja kwako."  Ufunuo 3:3.

Umilele wote kuamuliwa

 Kazi ya Hukumu ya Upelelezi itakapofungwa, UMILELE wa  [watu] wote utakuwa UMEAMULIWA, ama kwa UZIMA, ama kwa MAUTI [Hapatakuwa na nafasi nyingine tena ya kuhubiriwa Injili].  MUDA WA MAJARIBIO [KUPIMWA] unakoma kipindi kifupi tu KABLA ya kuonekana kwa Bwana wetu katika mawingu ya mbinguni [kuja kulinyakua Kanisa Lake]. Kristo, akiangalia mbele, anatangaza katika kitabu cha Ufunuo maneno haya: "Mwenye KUDHULUMU na AZIDI kudhulumu; mwenye UCHAFU na AZIDI kuwa mchafu; NA MWENYE HAKI NA AZIDI KUTAKASWA. Tazama, naja upesi, na UJIRA [MSHAHARA] wangu u pamoja nami [Warumi 6:23], KUMLIPA kila mtu  kama KAZI [MATENDO] yake ilivyo." Ufunuo 22:11,12. [2 Wathesalonike l:5-10].

 Wenye HAKI na WAOVU watakuwa bado wanaishi duniani katika hali yao inayokufa (mortal state) ----- watu watakuwa WAKIPANDA na KUJENGA, WAKILA na KUNYWA, wote wakiwa HAWANA HABARI kwamba HUKUMU YA MWISHO ISIYOBADILIKA [KUHUSU KESI ZAO] IMEKATWA na KUTANGAZWA katika PATAKATIFU PA MBINGUNI. Kabla ya Gharika, baada ya Nuhu kuingia katika safina, Mungu  AKAMFUNGIA NDANI na KUWAFUNGIA NJE WAOVU; walakini KWA SIKU SABA watu, PASIPOKUJUA, kwamba MAANGAMIZI yao yalikuwa  yameazimiwa, waliendelea na maisha yao ya KUTOJALI, maisha ya  ANASA na KUDHIHAKI maonyo ya hukumu iliyokuwa inawajia ghafula.  Mwokozi asema hivi: "Ndivyo kutakavyokuwa kuja Kwake Mwana wa Adamu." Mathayo 24:39. Kimya kimya, kama mwivi wa usiku wa manane, itakuja SAA ile ya kuamua MAMBO YOTE ambayo itashuhudia KUFUNGWA KWA UMILELE wa kila mwanadamu, na kuondolewa kwa mara ya mwisho MSAADA wake wa REHEMA kwa wanadamu wenye dhambi [wakati huo haitawezekana kutubu].

 "Kesheni basi... asije akawasili ghafula akawakuta mmelala [hamjajitayarisha]. Marko l3:35,36. Hali hii ni ya HATARI SANA  kwa [Wakristo] wale ambao, wakiwa WAMECHOKA KUKESHA, wanageukia VISHAWISHI vya ulimwengu huu. [Mathayo 24:42-5l].  Wakati mtu wa BIASHARA amezama [mawazo yake yote yako] katika KUTAFUTA FAIDA, wakati MPENDA ANASA anaendelea kutafuta kujiridhisha katika hiyo, wakati BINTI WA MITINDO anapanga MAPAMBO yake ----- huenda ni katika SAA hiyo HAKIMU WA DUNIA YOTE atakapotamka hukumu hii, "UMEPIMWA KATIKA MIZANI [AMRI KUMI] NAWE UMEONEKANA KUWA UMEPUNGUKA." Danieli 5:27.

 

 ----- E.G. White, in THE TRIUMPH OF GOD'S LOVE, Uk.284-290,  or THE GREAT CONTROVERSY, Uk. 480-491.

 

 ----- ( Facing our Life Record - Kiswahili ) -----

Kwa habari zaidi tafadhali tuandikie: 

Leaves of Life – International

                                                                        S.L.P. 17

                                                                                    Mafinga Iringa Tanzania