Masomo

Featured Image

NGUVU YA NENO

Biblia inacho kile kiwezacho kumfanya Mkristo kuwa na nguvu ya kiroho na kiakili.  Mtunga Zaburi asema hivi,  “Kuyafafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga.”  Zaburi 119:130.  Biblia ni kitabu cha ajabu.  Ni historia inayotufunulia sisi mambo ya karne zile zilizopita.  Pasipo kuwa na  Biblia, sisi tungekuwa tumeachwa kufuata dhana mbalimbali na hadithi za uongo kwa habari ya matukio ya vizazi vile vilivyopita.  Ni unabii unaolifunua pazia la siku zijazo.  Ni Neno la Mungu, liufunualo mpango ule wa wokovu, ambalo linatuonyesha njia ile ambayo kwayo  sisi tunaweza kuikwepa mauti ile ya milele, na kujipatia wema wa milele na uzima wa milele.  Katika vitabu vyote vinavyoigharikisha [vinavyoijaza] dunia hii, haidhuru viwe vya thamani ilioje, Biblia ni Kitabu kipitacho vitabu vyote, inastahili kabisa kuwa somo letu na kupewa heshima.  Haitupatii sisi historia ya ulimwengu huu tu, bali maelezo ya ulimwengu ule ujao.  Ina mafundisho yahusuyo maajabu ya malimwengu mbalimbali;  inatufunulia katika ufahamu wetu tabia ya Mwasisi yule wa mbingu na nchi.  Ndani yake umo ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Endelea kusoma

 

KUBADIRISHWA KWA NEEMA

Maombi ni njia iliyowekwa na Mbingu ya kupata ushindi katika pambano letu dhidi ya dhambi na katika kuikuza tabia yetu ya Kikristo.  Mivuto mitakatifu inayokuja kama jibu kwa maombi ya imani itafanikiwa kutenda kazi katika moyo wa mwombaji kwa kumpatia yale yote aombayo.  Kwa ajili ya kupewa msamaha wa dhambi, kwa ajili ya kupewa Roho Mtakatifu, kwa tabia ile inayofanana na ya Kristo, kwa ajili ya kupewa hekima na nguvu ili kufanya kazi yake, kwa kipawa cho chote alichotuahidi, tunaweza kuomba;  na ahadi yake ni hii,  “Mtapokea.”

     Ilikuwa ni katika mlima ule, akiwa pamoja na Mungu, Musa alipokiona kiolezo cha jengo lile la ajabu ambalo lilikusudiwa kuwa maskani ya kukaa utukufu wa Mungu.  Ni katika mlima tukiwa pamoja na Mungu  -  katika mahali petu pa faragha pa maombi  -    tunapopaswa kuutafakari mfano ule ulio bora kwa wanadamu.  Endelea kusoma

 

 

YANIPASA NIFANYE NINI ILI NIPATE KUOKOKA?

     Wakati ambapo wokovu wetu hutegemea kabisa juu ya Yesu, bado sisi tunayo kazi ya kufanya ili tupate kuokoka.  Mtume anasema,  “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.  Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:12,13).  Kazi tunayotakiwa kufanya si kazi ya kujitegemea wenyewe mbali na kazi ile anayotaka kufanya Mungu [ndani yetu], bali ni kazi ya kushirikiana na Mungu.  Uweza na Neema ya Mungu hutumiwa na Mtendakazi huyo wa Mbinguni ndani ya moyo;  lakini hapa ndipo wengine hupotea, wakidai kwamba mwanadamu anayo kazi ya kufanya ambayo ni ya kujitegemea mwenyewe kabisa bila kushirikiana na kazi yo yote anayotenda Mungu [ndani yake].  Kundi lingine huvuka mpaka na kwenda upande mwingine, na kusema kwamba mwanadamu hawajibiki kabisa, ati kwa sababu Mungu anafanya kazi yote  -  kutaka na kutenda.  Lakini sababu ya kweli tunayotakiwa kuifuata ni ile isemayo kwamba nia [mapenzi] ya mwanadamu inapaswa kuitii nia [mapenzi] ya Mungu.  Nia ya mwanadamu haipaswi kulazimishwa ili ipate kushirikiana na  wajumbe wale aliowaweka Mungu, bali inapaswa kunyenyekea kwa hiari.  Mwanadamu hana uwezo wo wote ndani yake wa kumwezesha kuutimiza wokovu wake mwenyewe.  Endelea kusoma