>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Bwana ni haki yetu

Bwana ni haki yetu

BWANA NI HAKI  YETU

     Kwa hiyo, swali ni hili,  Kwa jinsi gani inaweza kupatikana haki ile ambayo ni ya muhimu ili mtu aweze kuingia katika mji ule?  Kujibu swali hili ndiyo kazi kuu ya Injili.  Hebu kwanza tupate fundisho lenye kielelezo juu ya kuhesabiwa haki, au kupewa haki.  Ukweli huu unaweza kutusaidia kuielewa vizuri nadharia hii.  Mfano huo umetolewa katika Luka l8:9-l4, kwa maneno haya:-

     "Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.  Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.  Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake;  Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.  Mimi nafunga mara mbili kwa juma;  hutoa zaka katika mapato yangu yote.  Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,  Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.  Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule;  kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa."

     Kielelezo hiki kilitolewa kutuonyesha sisi jinsi gani hatuwezi au tunaweza kupata haki.  Mafarisayo hawajatoweka kabisa;  kuna wengi siku hizi wanaotegemea kuipata haki kwa matendo yao mema.  Wanajiamini wenyewe kwamba wao ni wenye haki.  Hawajisifu kwa wazi siku zote juu ya wema wao huo, bali huonyesha kwa njia zingine ya kwamba wanategemea haki yao wenyewe.  Labda roho ile ya Farisayo ---- roho ambayo ingesimulia kwa Mungu matendo mema ya mtu mwenyewe kama sababu ya kupewa upendeleo ---- mara kwa mara hupatikana sana na mahali po pote miongoni mwa wale wanaojiita Wakristo ambao hujisikia wameshushwa chini sana kwa ajili ya dhambi zao.      Wanajua kwamba wametenda dhambi, nao wanajisikia kuhukumiwa moyoni kuwa wanayo hatia.  Wanaomboleza juu ya hali yao ya dhambi, na kujutia udhaifu wao.  Ushuhuda wao haupandi juu ya usawa huo.  Mara nyingi wanajizuia kwa aibu nyingi sana wasiseme kitu cho chote katika mkutano wa kutoa ushuhuda, na mara nyingi hawathubutu kumkaribia Mungu kwa maombi.   Baada ya kutenda dhambi kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida, wanajitenga na maombi kwa muda fulani, mpaka imepita ile hali ya kujisikia vibaya kwa kushindwa kwao, ama mpaka wanapofikiri kwamba wamefidia kwa kuwa na tabia maalum njema.  Hii ni ishara ya nini? ---- Ya roho ile ya Kifarisayo ambayo ingeweza kutamba kwa ajili ya haki yake yenyewe mbele  za Mungu;  ambayo haiwezi kuja mbele Zake mpaka kwanza ijitegemeze kwa mkongojo  wa uongo wa wema wake unaodhaniwa tu.  Wanataka waweze kumwambia  Bwana, "Tazama jinsi nilivyoweza kuwa mwema kwa siku chache zilizopita; hakika utanikubali  mimi sasa."

     Lakini matokeo yake ni nini? ----  Mtu yule aliyeitegemea haki yake mwenyewe hakuwa nayo, ambapo mtu yule aliyeomba kwa majuto yatokayo moyoni kwa ajili ya dhambi zake, akisema,   Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,"  alishuka kwenda nyumbani kwake akiwa mtu mwenye haki.  Kristo anasema kwamba alikwenda akiwa AMEHESABIWA HAKI, yaani, amefanywa kuwa mwenye haki.

     Zingatia kwamba yule mtoza ushuru alifanya jambo fulani la ziada kuliko kujililia tu uovu wake;  aliomba rehema.  Rehema ni nini? ---- Ni upendeleo ambao mtu hastahili kupewa.  Ni moyo ule wa kumtendea mtu vizuri zaidi  kuliko  vile anavyostahili.  Sasa lile Neno lenye Pumzi ya Mungu linasema hivi juu ya Mungu:  "Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,  kadiri ile ile rehema Zake ni kuu kwa wamchao."  Zab.l03:ll.  Yaani, kile kipimo ambacho Mungu anatumia anapotutendea sisi vizuri zaidi kuliko vile tunavyostahili tunapokuja kwake kwa unyenyekevu, ni sawa na umbali uliopo kati ya nchi na mbingu ya juu mno.  Ni kwa jinsi gani Anatutendea sisi vizuri kuliko vile tunavyostahili?  ----  Kwa kuziondoa dhambi zetu mbali nasi;  kwa maana fungu linalofuata linasema:  "Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo Alivyoweka dhambi zetu mbali nasi."  Maneno ya mwanafunzi aliyependwa sana yanakubaliana na maneno hayo:  "Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote."  l Yohana l:9.

     Kwa maelezo zaidi juu ya rehema yake Mungu, na jinsi inavyodhihirishwa, soma Mika 7:l8,l9:  "Ni nani aliye Mungu kama Wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia?  hashiki hasira yake  milele, kwa maana Yeye hufurahia rehema.  Atarejea na kutuhurumia;  Atayakanyaga maovu yetu;  Nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari."  Hebu sasa na tusome usemi wa moja kwa moja kutoka katika Maandiko juu ya jinsi haki hii inavyotolewa.

     Mtume Paulo, baada ya kuthibitisha kwamba wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu kiasi kwamba hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria, anaendelea kusema kwamba tuna"hesabiwa haki [tunafanywa kuwa wenye haki] bure kwa neema Yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu,  ambaye Mungu amekwisha kumweka awe  upatanisho kwa njia ya imani katika damu Yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa;  apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe Mwenye haki na Mwenye kumhesabia haki  yeye amwaminiye Yesu."  Rum.3:24-26.

     "Kufanywa kuwa wenye haki bure."  Ingekuwaje vinginevyo?  Kwa kuwa juhudi zilizo bora sana za mtu mwenye dhambi hazina matunda hata kidogo kuweza kuleta haki, basi, ni wazi kwamba njia pekee ambayo kwayo inaweza kuja kwake ni kama kipawa.  Kwamba haki ni kipawa inaelezwa kwa wazi na Paulo katika Warumi 5:l7:  "Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo."  Ni kwa sababu haki ni kipawa kwamba nao uzima wa milele, ambao ni kipawa cha haki, ni kipawa cha Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

     Kristo amewekwa mbele yetu na Mungu kama ndiye ambaye kupitia kwake msamaha wa dhambi unaweza kupatikana;  na msamaha huu umejengwa tu katika tangazo la haki Yake (ambayo ndiyo haki yake Mungu) kuwa ndiyo ondoleo la dhambi.  Mungu "kwa kuwa ni mwingi wa rehema" (Efe.2:4), na ambaye hufurahia rehema, anaweka haki Yake Mwenyewe juu ya mwenye dhambi anayemwamini Yesu, kama Aliye badala yake kwa ajili ya dhambi zake.  Hakika, huko ni kubadilishana kwenye manufaa kwa mwenye dhambi, wala sio hasara kwa Mungu, kwa kuwa kwake Yeye utakatifu Wake hauna kikomo, wala akiba yake haiwezi kupungua kamwe.

     Maandiko ambayo tumekuwa tukiyatafakari sasa hivi (Rum.3:24-26) ni usemi mwingine tu wa mafungu 2l, 22, kufuatia tangazo kwamba hakuna mwenye mwili atakayefanywa kuwa mwenye haki kwa matendo ya sheria.  Mtume anaongeza kusema:  "Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria;  inashuhudiwa na torati na manabii;  ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio,"  Mungu anaweka haki yake juu ya muumini.  Anamfunika nayo, hata dhambi yake haionekani tena.  Ndipo huyo aliyesamehewa awezapo kushangilia pamoja na nabii:-

     "Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu;  maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu."  Isa.6l:l0.

     Lakini ni vipi ilivyo "haki ya Mungu pasipo sheria"?  Hiyo inakubalianaje na usemi usemao kwamba sheria ndiyo haki ya Mungu;  na ya kwamba nje ya matakwa yake hakuna haki?  Hapa hakuna kupingana.  Sheria haipuzwi kwa njia hii.  Angalia kwa makini:  Ni nani aliyeitoa sheria?  ----  Kristo.  Aliitangazaje?  ----  "Kama Mmoja aliye na mamlaka," kama vile Mungu.  Sheria ilitoka Kwake kama ilivyotoka kwa Baba, nayo ni tangazo tu la haki ya tabia Yake.  Kwa hiyo, haki inayopatikana kwa imani katika Yesu Kristo ni ile ile iliyofupishwa katika sheria;  na jambo  hilo linathibitishwa zaidi kwa ukweli kwamba "inashuhudiwa na torati [sheria]."

     Hebu msomaji ajaribu kupiga picha ya mandhari hii.  Hapa inasimama sheria ambayo ni shahidi aliye tayari kabisa kutoa ushahidi wake dhidi ya mwenye dhambi.  Haibadiliki, wala haitamwita mwenye dhambi kuwa ni mwenye haki.  Mwenye dhambi huyu aliyethibitishiwa hatia yake anajaribu tena na tena kupata haki kutoka kwa sheria hiyo,  lakini inapinga juhudi zake zote za kuikaribia.  Haiwezi kuhongwa kwa  kiasi cho chote kile cha adhabu ya kumfanya atubu [penance] au kwa matendo yanayokubalika kuwa ni mema.  Lakini hapa anasimama Kristo, "amejaa neema" pamoja na kweli, naye anamwita mwenye dhambi kwake.  Hatimaye mwenye dhambi huyu, akiwa amechoka sana kwa juhudi yake ya bure ya kupata haki kutoka kwa ile  sheria, anasikiliza sauti ya Yesu, na kukimbilia katika mikono yake iliyonyoshwa kuelekea kwake.  Akijificha ndani ya Kristo, anafunikwa na haki Yake;  na sasa, tazama!  Kwa njia ya imani katika Kristo amejipatia kile alichokuwa amejitahidi bure kukipata.  Anayo  haki ambayo sheria inaitaka, nayo ni kitu halisi, kwa  sababu kimepatikana kutoka kwa yule aliye Chimbuko la Haki;  kutoka mahali pale pale ilipotoka sheria.  Na sheria nayo inashuhudia uhalali wa haki yake.  Inasema kwamba kwa kadiri mtu huyo anavyokuwa nayo, basi, itakwenda mahakamani na kumtetea dhidi ya washtaki wake wote.  Itashuhudia ukweli kwamba yeye ni mtu mwenye haki.  Pamoja na kuwa na haki ile ipatikanayo "kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu" (Wafilipi 3:9), Paulo alikuwa na hakika kwamba atasimama imara katika siku ile ya kuja Kristo.

     Hakuna sababu yo yote katika tendo hilo ya kulitoa makosa.  Mungu ni mwenye haki, na Mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.  Ndani ya Yesu unakaa utimilifu wote  wa Mungu;  Yeye yu sawa na Baba Yake katika kila tabia.  Kwa sababu hiyo, ukombozi uliomo ndani yake  ----    uwezo ule wa kumnunua tena mwanadamu aliyepotea  ----  ni wa milele.  Uasi wa mwanadamu ni kinyume na Mwana kama ulivyo kinyume na Baba, maana hao wawili ni umoja.  Kwa hiyo, Kristo "alipojitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu, "alikuwa ni Mfalme akiteseka kwa maasi ya raia zake" ----  Yule aliyejeruhiwa akipita na kuliachilia kosa la mkosaji.  Hakuna ye yote mwenye mashaka atakayekana kwamba mtu ye yote anayo haki na upendeleo wa kusamehe kosa lo lote alilotendewa;  basi, kwa nini kubishana bila kuwa na sababu za kutosha Mungu anapotumia haki iyo hiyo?  Hapana shaka lo lote kwamba kama Akitaka kusamehe madhara Aliyotendewa Mwenyewe, anayo haki kufanya hivyo;  na zaidi sana kwa kuwa anaithibitisha haki ya sheria Yake kamilifu kwa kuchukua katika nafsi Yake Mwenyewe adhabu ile aliyostahili yule mwenye dhambi.   "Lakini yule asiyekuwa na hatia aliteseka kwa ajili ya wenye hatia."  Ni kweli;  ila yule Mteswa Asiyekuwa na hatia "alijitoa Mwenyewe" kwa hiari, ili apate kufanya haki kwa Serikali Yake kwa kufanya kile ambacho upendo wake ulimsukuma kufanya, yaani, kuyaachilia madhara aliyotendewa Mwenyewe kama Mtawala wa Ulimwengu wote.

     Sasa soma maneno ya Mungu Mwenyewe kulihusu Jina lake Mwenyewe  ----  maneno yaliyotolewa wakati wa tukio baya mno la dharau iliyopata kuonyeshwa Kwake:-

     "BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la  BWANA.  BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa  huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu,

mwenye kusamehe uovu na makosa na  dhambi;  wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe;  mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne."  Kut.34:5-7.

     Hili ndilo Jina lake Mungu;  ni katika tabia Yake anamojidhihirisha Mwenyewe kwa mwanadamu;  Yeye ndiye nuru anayotaka watu waiangalie.  Lakini inakuwaje  kwa lile tangazo lake lisemalo kwamba  "Wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe?"   Hilo linakubaliana  kabisa na tabia yake ya kutokuwa mwepesi wa hasira, kuwa mwingi wa rehema na kweli, na kule kuachilia kwake makosa ya watu Wake.  Ni kweli kwamba Mungu hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe;  asingeweza kufanya hivyo na bado awe Mungu mwenye haki.  Lakini anafanya jambo fulani ambalo ni bora zaidi:  "ANAIONDOA HATIA, ili yule ambaye hapo kwanza alikuwa na hatia asihitaji tena kuondolewa hatia hiyo,  ----  anahesabiwa haki, na kuhesabiwa kana kwamba hajapata kutenda dhambi kamwe.

     Hebu asiwepo mtu ye yote anayebisha juu ya maneno haya "kuvikwa haki," kana kwamba jambo hilo ni unafiki.  Wengine, waliopungukiwa na shukrani kwa thamani ya kipawa hiki cha haki, wamesema kwamba wao hawakutaka haki "ya kuvikwa", bali kwamba  walitaka haki ile inayotokana tu na maisha yao, hivyo wanaikashifu haki ya Mungu, lambayo ni kwa njia ya imani katika Yesu Kristo KWA wote na JUU YA wote waaminio.   tunaliafiki wazo lao kwa upande ule tu unaopinga unafiki, lyaani, ule mfano wa utauwa unaokana nguvu Zake;  lakini tungependa msomaji azingatie wazo hili akilini mwake:  Inaleta tofauti kubwa sana kuhusu nani anayehusika KUTUVIKA HAKI hiyo.  Kama ni sisi tunaojaribu kujivika wenyewe, basi, hatupati kabisa kitu cho chote juu yetu, ila nguo iliyotiwa unajisi tu, haidhuru ionekane nzuri kiasi gani kwetu;  bali Kristo anapotuvika sisi nayo, hapo haipaswi kudharauliwa wala kukataliwa.  Zingatia maneno ya Isaya:  "Amenifunika vazi la haki."  Haki ile  anayotufunika Kristo ndiyo inayokubalika na Mungu;  na iwapo Mungu ameridhika nayo, bila shaka wanadamu wasingejaribu kupata kitu kingine cho chote kizuri zaidi.

     Lakini, basi, tutauendeleza mfano huu kwa hatua moja zaidi, na jambo hili litaliondolea suala hili utata wote.  Zekaria 3:l-5 anatoa suluhisho;  mafungu hayo yanasomeka hivi:

     "Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa BWANA, na Shetani amesimama mkono wake  wa kuume ili kushindana naye.  BWANA akamwambia Shetani,  BWANA na akukemee,  Ewe Shetani;  naam, BWANA, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee;  je!  hiki si kinga kilichotolewa motoni?  Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele  ya malaika.  Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu.  Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.  Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi;  naye malaika wa BWANA akasimama karibu."

     Angalia katika kisa hicho juu kwamba kitendo cha kumvua nguo zile zenye uchafu ni kitendo kile  kile cha kuondoa uovu wa mtu huyo.  Basi, tunaona kwamba Kristo  anapotufunika na vazi la haki Yake, hatuviki joho la kufunika dhambi yetu, bali kwanza anaiondolea mbali dhambi hiyo.  Jambo hilo linaonyesha kwamba msamaha wa dhambi ni zaidi  ya mfano, ni zaidi ya kuandika tu katika vitabu vya kumbukumbu mbinguni kuwa dhambi hiyo imefutwa.  Msamaha wa dhambi ni kitendo halisi;  ni kitu kinachoonekana wazi, ni kitu kinachomwathiri kabisa mtu.  Huo [msamaha] unamwondolea kabisa hatia;  na kama ameondolewa hatia yake, basi, amehesabiwa haki, amefanywa kuwa mwenye  haki, hapana budi atakuwa amepitia badiliko kubwa sana.  Naam, yeye ni mtu mwingine.  Kwa maana aliipata haki hii kwa ondoleo la dhambi zake katika Kristo.  Ilipatikana tu kwa kumvaa Kristo.  Walakini,  "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe  kipya."  2 Kor.5:l7.  Basi, msamaha huo ulio kamili, utolewao bure, ndani yake unakuwa  na badiliko lile la ajabu na la kimiujiza liitwalo kuzaliwa upya;  maana mtu hawezi kuwa kiumbe kipya isipokuwa  kwa kuzaliwa upya.  Hii ni sawasawa na  kuwa na moyo mpya, ama moyo safi.

     Moyo mpya ni moyo ule unaoipenda haki na kuichukia dhambi.  Ni moyo ulio tayari kuongozwa katika njia za haki.  Ni moyo kama huo ambao Bwana alitamani Israeli wawe nao aliposema,  "Laiti wangekuwa na moyo kama huu ndani yao siku zote, wa kunicha, na kushika amri zangu zote siku zote, wapate kufanikiwa wao na watoto wao milele!"  Kum.5:29.  Kwa kifupi, ni moyo ule usiopenda dhambi na uliowekwa huru kutokana na hatia ya dhambi.  Lakini ni kitu gani hasa kinachomfanya mtu atamani kwa dhati msamaha wa dhambi zake?  ----  Ni ile chuki yake tu kwa dhambi hizo, na tamaa yake kwa ile haki, chuki na tamaa vyote viwili vikiwa vimechochewa na Roho Mtakatifu.

     Roho hushindana  na wanadamu wote.  Anakuja kama Mmoja alaumuye dhambi;  sauti yake ya karipio inapojaliwa, basi, mara moja anaanza kazi yake kama Mfariji.  Moyo ule ule wenye kunyenyekea na kujitoa  unaomwongoza mtu huyo kulipokea karipio la Roho, pia utamwongoza kuyafuata mafundisho ya Roho, na ndipo hapo Paulo husema    kwamba  "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu."  Rum.8:l4.

     Tena, ni kitu gani hasa kinacholeta kuhesabiwa haki, au msamaha wa dhambi?  Ni ile imani, kwa maana Paulo asema:  "Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na  amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo."  Rum.5:l.  Haki ya Mungu inatolewa kwa na kuwekwa juu ya kila mmoja aaminiye.  Rum.3:22.  Lakini   zoezi lili hili la imani ndilo linalomfanya mtu kuwa mwana wa Mungu;  maana, asema tena mtume Paulo "kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu."  Gal.3:26.

     Ukweli kwamba kila mmoja ambaye dhambi zake zimesamehewa papo hapo anakuwa mwana wa Mungu, huonekana katika Waraka wa Paulo kwa Tito.  Kwanza anaonyesha hali ya uovu ambayo tulikuwa nayo zamani, kisha asema (Tito 3:4-7):-

     "Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;  si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi;  bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa  pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu;  ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu."

     Zingatia ya kwamba ni kwa kuhesabiwa haki kwa neema yake sisi tunafanywa warithi.  Tumekwisha kujifunza tayari kutoka kwa Warumi 3:24,25 kwamba kuhesabiwa haki huku kwa neema yake ni kwa njia ya imani yetu katika Kristo;  lakini Wagalatia 3:26 hutuambia kuwa imani hii katika Kristo Yesu ndiyo inayotufanya sisi kuwa wana wa Mungu;  basi, tunajua ya kwamba ye yote ambaye amehesabiwa haki kwa neema ya Mungu,  ----  amesamehewa,  ----  ni mwana na mrithi wa Mungu.

     Hii huonyesha kwamba hakuna sababu kwa wazo lisemalo kwamba sharti mtu apitie kipindi fulani cha majaribio,  naye afikie kiwango fulani cha utakatifu kabla Mungu hajamkubali kama mwana wake.  Anatukubali jinsi tulivyo.  Si kwa ajili  ya wema wetu kwamba anatupenda sisi, bali ni kwa sababu ya hitaji letu.  Anatupokea, si kwa ajili ya kitu  kingine cho chote alichokiona ndani yetu, bali  kwa ajili Yake Mwenyewe, na kwa kile ajuacho kwamba uweza wake wa Uungu  unaweza  kutufanyia sisi.  Ni wakati ule tu tunapoutambua ukuu wake wa ajabu na utakatifu wake Mungu, pamoja na ukweli kwamba anakuja kwetu tukiwa katika hali yetu ya dhambi na ya kuaibisha, ili apate  kutuingiza katika familia Yake, hapo ndipo tunapoweza kuthamini nguvu ya maneno ya mshangao ya mtume,  "Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu."  l Yohana 3:l.  Kila  mmoja aliyepewa heshima hii, atajitakasa mwenyewe, kama Yeye alivyo  mtakatifu.

     Mungu hatuiti sisi wana wake kwa sababu sisi tu wema, bali ili atufanye sisi kuwa wema.  Asema Paulo:  "Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi Yake makuu aliyotupenda;  hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa  yetu; alituhuisha [alitufanya sisi kuwa hai] pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;  ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika  Kristo Yesu."  Efe.2:4-7.  Kisha anaongeza, na kusema, "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;  wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.  Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo."  Fungu la 8-l0.  Kifungu hiki kinaonyesha kwamba Mungu alitupenda  sisi tulipokuwa wafu kwa sababu ya dhambi zetu;  Yeye Anatupa sisi Roho Wake ili kutufanya tuwe hai katika Kristo, na Roho yule yule anatupiga chapa na kutuingiza katika familia ya Mungu;  na hivyo anatuchagua sisi, kama viumbe vipya katika Kristo, ili tupate kufanya matendo mema ambayo Mungu ameyatengeneza.