>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Haki ya Mungu

Haki ya Mungu

HAKI YA MUNGU

     "Bali utafuteni kwanza ufalme Wake, na haki yake;  na hayo yote mtazidishiwa."  Mt.6:33.

     Haki ya Mungu, asema Yesu,  ndicho kitu kimoja tu cha kutafutwa katika maisha  haya.  Chakula na mavazi ni mambo madogo ukilinganisha nacho.  Mungu atatupatia hivyo vyote; kama jambo la kawaida, hata isiwepo haja kwetu sisi kujisumbua na kuwa na wasiwasi juu yake;  walakini kutafuta ufalme wa Mungu na haki Yake lingekuwa ndilo lengo la pekee la maisha yetu.

     Katika l Wakorintho l:30 tunaambiwa ya kwamba Amefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu; na kwa vile Kristo ni hekima ya Mungu, na ndani Yake unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili, ni dhahiri kwamba haki ile anayofanywa kwetu ni haki ya Mungu.  Hebu tuone haki hiyo ni nini.

     Katika Zaburi ll9:l72 Mtunga  Zaburi anamwambia Bwana:  "Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo [amri] yako yote ni ya haki.  Maagizo [amri] ni haki, sio tu kinadharia, bali ni haki ya Mungu hasa.  Kwa ushahidi hebu soma yafuatayo:-

     "Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini;  maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika;  bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka.  Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao."  Isa.5l:6,7.

     Tunajifunza nini kutokana na maneno hayo? ---- Ya kwamba wale waijuao haki ya Mungu ni wale ambao mioyoni mwao imo sheria Yake,  basi, sheria ya Mungu ndiyo haki ya Mungu.

     Jambo hili laweza kuthibitishwa tena kama ifuatavyo:  "Kila lisilo la haki ni dhambi."  l Yohana 5:l7.  "Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria."  l Yohana 3:4, AJKK.  Dhambi ni uvunjaji wa sheria ya Mungu, tena ni kila lisilo la haki;  kwa hiyo dhambi na kila lisilo la haki ni mambo mawili yanayofanana.  Lakini kama lile LISILO LA HAKI ni uvunjaji wa sheria ya Mungu, basi,haki lazima iwe ni ule utii kwa sheria ya Mungu.  Ama, tuliweke azimio hili katika mfumo wa mahesabu:-

"Lisilo la haki = dhambi.  l Yohana 5:l7. Uvunjaji wa Sheria ya Mungu =  dhambi. " l Yohana 3:4, (AJKK.)

     Kwa hiyo, kulingana na msimamo unaokubaliwa na wote wenye akili ni kwamba mambo mawili yakiwa sawa na jambo moja lile lile, basi, yanakuwa sawa kila moja kwa jingine, hivyo tunapata:-

                                 Lisilo la haki = Uvunjaji wa Sheria ya Mungu

huo ni mlinganyo hasi (negative equation).  Jambo lilo hilo, likiwekwa katika maneno yenye chanya (positive), yangekuwa hivi:-

                                            Haki = Utii kwa Sheria ya Mungu.

     Sasa, ni sheria ipi ambayo utii kwake ni haki na uvunjaji wake ni dhambi?  Ni sheria ile isemayo,  "Usitamani;" kwa maana mtume Paulo anatuambia  ya kwamba ni sheria hiyo iliyomjulisha dhambi yake.  Rum.7:7.  Sheria ile ya Amri Kumi, basi, ndicho kipimo cha haki ya Mungu.  Kwa kuwa sheria ya Mungu nayo ni haki, bila shaka hiyo ndiyo haki ya Mungu.   Kwa kweli, hakuna haki nyingine yo yote.

     Kwa kuwa sheria ndiyo haki ya Mungu ---- nakala ya tabia Yake ---- ni rahisi kuona kwamba kumcha Mungu na kushika amri Zake ndiyo impasayo mtu.  Mhu.l2:l3.  Hebu asiwepo mtu ye yote anayedhani kwamba wajibu wake utakuwa umewekewa mipaka ukifungwa kwa zile amri kumi tu, maana amri hizo ni "pana mno." "Torati [sheria] ni ya rohoni," nayo ina mambo mengi sana ndani yake kuliko  yanavyoweza kutambulikana na msomaji wa vivi hivi tu.  "Basi mwanadamu wa tabia ya asili  hayapokei mambo ya Roho wa Mungu;  maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni."  l Kor.2:l4.  Upana mno wa sheria ya Mungu unaweza kufahamika tu na wale waliokwisha kutafakari  juu  yake kwa maombi.  Mafungu machache tu ya  Maandiko yatatosha kutuonyesha sisi jambo fulani juu ya upana wake.

     Katika hotuba yake mlimani Kristo alisema:  "Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue;  na mtu akiua, itampasa hukumu.  Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira,itampasa hukumu;  na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza;  na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto."  Mt.5:2l,22.  Na tena:  "Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;  lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake."  Fungu la 27, 28.

     Hii haina maana kwamba amri, "Usiue," na "Usizini,' hazijakamilika, ama kwamba sasa Mungu anataka kiwango kikubwa zaidi cha uadilifu kutoka kwa watu wake walioitwa Wayahudi.  Anataka kiwango kile kile katika vizazi vyote.  Mwokozi alikuwa anazifafanua tu amri hizi, na kuonyesha hali  yake kiroho.  Kwa shutuma isiyotamkwa ya Mafarisayo, kwamba alikuwa haijali na kuihafifisha sheria hii ya maadili, Alijibu kwa kusema kwamba Yeye alikuja kwa kusudi la kuithibitisha sheria hiyo, na ya kwamba isingeweza kutanguliwa;  kisha akawaeleza maana halisi ya sheria hiyo kwa njia ambayo iliwasadikisha kwamba wao ndio hawakuijali wala kuitii.  Aliwaonyesha kwamba hata kwa kutazama tu au kwa wazo tu uvunjaji wa sheria hiyo ungeweza kutokea, na kwamba kwa kweli inayatambua hata mawazo  na makusudi ya moyo.

     Katika suala hili, Kristo hakufunua ukweli mpya, bali aliwajulisha na kuwafunulia tu ule ule wa zamani.  Sheria ilikuwa na maana ile ile wakati ule alipoitangaza pale Sinai na wakati alipoifafanua juu ya mlima ule kule Yudea.  Wakati ule, kwa sauti yake iliyoitetemesha nchi, aliposema, "Usiue," alimaanisha, "Usitunze  hasira moyoni;  usiwe na wivu, wala ugomvi, wala kitu cho chote kinachofanana na kuua."  Yote haya na  zaidi yake yamo katika maneno yasemayo, "Usiue."  Na jambo hilo lilifundishwa kwa maneno yaliyovuviwa ya Agano la Kale;  kwa maana Sulemani alionyesha kwamba sheria inashughulika na mambo yasiyoonekana  pamoja na yale yanayoonekana, hapo alipoandika hivi:

     "Hii ndiyo jumla ya maneno, yote yamekwisha sikiwa;  Mche Mungu, nawe uzishike amri Zake,  Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.  Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.  Mhu.l2:l3,l4

     Hoja ni hii:  Hukumu inapitishwa juu ya kila  neno la siri;  Sheria ya Mungu ndicho kipimo katika hukumu hii, ----  inakadiria sifa ya kila tendo, likiwa jema au likiwa baya;  kwa hiyo, sheria ya Mungu hukataza uovu katika mawazo na katika matendo pia.  Basi, jumla ya maneno yote ni kwamba amri za  Mungu zina yote yampasayo mtu kufanya.

     Chukua amri ya kwanza,  "Usiwe na miungu mingine ila Mimi."  Mtume anatueleza sisi habari ya wengine ambao "mungu wao ni tumbo."  Wafilipi 3:l9.  Walakini ulafi na ulevi ni kujiua mwenyewe;  na kwa ajili hiyo tunaona ya kuwa amri ya kwanza inapitiliza kwenda hadi amri ya sita.  Lakini haya si yote, kwa maana anatueleza pia kuwa kutamani ni ibada ya sanamu.  Kol. 3:5.  Amri ya Kumi haiwezi kuvunjwa pasipo kuivunja ile ya  kwanza na ya pili.  Kwa maneno mengine, amri ya kumi ni sawa na ile ya kwanza;  nasi tunaona ya kwamba Amri Kumi ni kama duara  ambayo mzingo wake ni mkubwa  sawasawa na ulimwengu wote, na ndani yake umo wajibu wa kimaadili kwa kila kiumbe.  Kwa kifupi, ni kipimo cha haki ya Mungu, aishiye milele.

     Mambo yakiwa hivyo, basi, usahihi wa usemi ule usemao kwamba "wale waitendao sheria watahesabiwa haki," ni dhahiri.  KUHESABIA HAKI  maana yake KUMFANYA MTU AWE NA HAKI, ama ni kumwonyesha mtu huyo kuwa ni mwenye haki.  Sasa, basi, ni dhahiri kwamba utii mkamilifu kwa sheria iliyo kamilifu ungemfanya mtu huyo kuwa mwenye haki.  Hili ndilo lilikuwa kusudi lake Mungu kwamba utii kama huo ungetolewa kwa sheria yake na viumbe vyake vyote;  na kwa njia hii sheria ilikuwa imeamriwa ipate kutuletea uzima.  Rum.7:l0.

     Lakini ili mtu aweze kupimwa kuwa ni "mtendaji wa sheria" ingekuwa lazima kwamba awe ameitunza sheria hiyo katika ukamilifu wake kwa kila dakika ya maisha yake yote.  Kama alipungua kufikia kiwango hicho, basi, asingeweza kusemwa kuwa aliitenda  sheria hiyo.  Asingeweza kuwa mtendaji wa sheria kama angekuwa ameitenda kwa sehemu tu.  Kwa hiyo, ni jambo la kusikitisha sana kwamba katika taifa lote la kibinadamu hakuna waitendao sheria, kwa maana Wayahudi na Watu wa Mataifa wote wako "chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa,  ya kwamba, Hakuna  mwenye haki hata mmoja.  Hakuna afahamuye;  Hakuna amtafutaye Mungu.  Wote wamepotoka, wameoza wote pia;  Hakuna mtenda mema, la! hata mmoja."  Rum.3:9-l2.  Sheria inanena kwa wote walio katika mazingira yake;  na katika ulimwengu wote hakuna hata mmoja awezaye kufunua kinywa chake ili kujinasua na shtaka la dhambi ambalo linaletwa juu yake.  Kila kinywa kimefumbwa, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu (fungu la l9),  "kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu" (fungu la 23).

     Basi, ijapokuwa wale "waitendao sheria watahesabiwa haki,"  ni dhahiri vile vile kwamba "hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria;  kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria."  Fungu la 20.  Sheria, ambayo ni "takatifu, na ya haki, na njema," haiwezi kumhesabia haki mwenye dhambi.  Kwa maneno mengine, sheria ya haki haiwezi kumtangaza yule anayeivunja kuwa hana hatia.  Sheria ile ambayo ingemhesabia haki mtu mwovu ingekuwa ni sheria potovu.  Sheria haipaswi kushutumiwa kwa sababu haiwezi kuwahesabia haki wenye dhambi.  Kinyume chake, inapaswa kusifiwa kwa  sababu hiyo.  Ukweli kwamba sheria haitaweza kuwatangaza wenye dhambi kuwa ni wenye haki, ----  kwamba haitaweza kusema kwamba watu wameishika wakati wao wameivunja, ---- huo peke yake ndio ushahidi wa kutosha kwamba ni njema.  Watu humsifu na kumpigia makofi hakimu mnyofu wa kidunia, ambaye hawezi kupokea rushwa, na ambaye hatamtangaza mtu mwenye hatia kuwa hana hatia.  Kwa kweli, wangepaswa kuisifu sheria ya Mungu, ambayo haitatoa ushuhuda wa uongo.  Hiyo ndiyo ukamilifu wa haki, na kwa hiyo inalazimika kutangaza ukweli ule wa kusikitisha kwamba hakuna hata mmoja wa ukoo wa Adamu aliyetimiza matakwa yake.

     Aidha, ukweli usemao kwamba kuitenda sheria ndiwo wajibu wa mwanadamu huonyesha kwamba anapopunguka katika jambo moja tu hawezi kamwe kulifidia.  Matakwa ya kila amri ya sheria hii ni mapana mno, ---- sheria yote ni ya kiroho mno, --- hata malaika angeweza tu kutoa sio zaidi ya utii wa kawaida.  Naam, zaidi ya hayo, sheria ni haki ya Mungu, ---- nakala ya tabia yake, ---- na kwa kuwa tabia Yake haiwezi kuwa tofauti na vile ilivyo hasa, inafuata ya kwamba hata Mungu Mwenyewe hawezi kuwa mwema zaidi ya kipimo cha wema kinachodaiwa na sheria Yake.  Hawezi kuwa mwema kuliko vile Alivyo, na sheria inamtangaza Yeye alivyo.  Kuna tumaini gani, basi, kwa yule aliyeshindwa, hata kwa amri moja tu, kuweza kuongeza wema wa ziada kutosha kujaza kipimo hiki kikamilifu?  Yule anayejaribu kufanya hivyo anajiwekea mbele yake kazi isiyowezekana ya kutaka kuwa bora kuliko vile Mungu anavyotaka, naam, hata kuwa bora kuliko Mungu Mwenyewe.

     Lakini sio katika jambo moja tu ambalo wanadamu wameshindwa.  Wamepungukiwa katika kila jambo.  "Wote wamepotoka, wameoza wote pia;  Hakuna mtenda mema, la! hata mmoja."  Si hivyo tu, bali haiwezekani kwa mwanadamu aliyeanguka dhambini, pamoja na uwezo wake duni, kufanya hata tendo moja tu linalofikia kiwango kile cha ukamilifu.  Azimio hili halihitaji ushahidi wa ziada kuliko kurudia usemi usemao ya kwamba sheria ndicho kipimo cha haki ya Mungu.  Kusema kweli, hakuna watu walio na ufidhuli kama ule wa wale wanaodai kwamba tendo lo lote la maisha yao limekuwa ama lingeweza kuwa jema kama vile ambavyo angefanya Bwana Mwenyewe.  Kila mmoja hana budi kusema pamoja na Mtunga Zaburi, "Sina wema ila utikao Kwako."  Zab. l6:2.

     Ukweli huu umo katika usemi wa moja kwa moja unaotoka katika Maandiko.  Kristo, ambaye "hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu;  kwa maana Yeye Mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu" (Yohana 2:25);  alisema:  "Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.  Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi."   Marko 7:2l-23.  Kwa maneno mengine, ni vyepesi kufanya mabaya kuliko kufanya mema, na mambo yale afanyayo mwanadamu kwa kawaida ni maovu.  Uovu unakaa ndani, nao umekuwa sehemu ya mtu huyo.  Basi, mtume asema:  "Kwa kuwa ile nia ya mwili ni  uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.  Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu."  Rum.8:7,8.  Na tena asema:  "Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili;  kwa maana hizi zimepingana hata  hamwezi kufanya mnayotaka."  Gal.5:l7.  Kwa kuwa uovu ni sehemu halisi ya asili ya mwanadamu,  umerithiwa na kila mtu kutoka  kwenye msururu mrefu wa mababu wenye dhambi, basi, ni dhahiri kabisa  kwamba haki yo yote inayotoka ndani yake itakuwa tu kama "nguo iliyotiwa unajisi" (Isa.64:6), ukilinganisha na lile vazi takatifu lisilokuwa na waa la haki ya Mungu.

     Kutokuwezekana huku kwa matendo mema kutoka ndani ya moyo wenye dhambi kunaelezwa kwa mfano na Mwokozi kwa mkazo huu:  "Kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake;  maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu.  Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu;  kwa kuwa mtu, kinywa  chake hunena yale yaujazayo moyo wake."  Luka 6:44,45.  Hii ni kusema kwamba, mtu hawezi kufanya mema mpaka kwanza awe mwema..  Kwa ajili hiyo, matendo yale yaliyofanywa na mtu mwenye dhambi hayana matokeo yo yote katika kumfanya awe mwenye haki, ni maovu tu, na hivyo yanaongezwa juu ya uovu wake wote.  Ni uovu tu unaoweza kutoka ndani ya moyo mwovu, na maovu yaliyozidishwa hayawezi kufanya tendo jema hata moja;  kwa hiyo ni bure kabisa kwa mtu mwovu kufikiri kuwa anaweza kuwa mwenye haki kwa juhudi zake mwenyewe.  Ni lazima kwanza afanywe kuwa mwenye haki kabla hajaweza kuanza kufanya mema yanayotakiwa kutoka kwake, ambayo yeye anataka kufanya.

     Shauri hili sasa linasimama hivi:  l.  Sheria ya Mungu ni haki kamilifu;  na utii kamili kwayo unatakiwa kwa kila mmoja atakayeingia katika ufalme wa mbinguni.  2.  Walakini sheria haina tone hata moja la haki  ya kumgawia mtu ye yote, kwa maana wote ni wenye dhambi, nao hawawezi kuyatimiza matakwa yake.  Haidhuru ni kwa bidii kiasi gani au kwa nguvu kiasi gani mtu anafanya kazi, hakuna lo lote awezalo kulifanya litakalotimiza kipimo hicho kamili kinachodaiwa na sheria.  Kiko juu mno kwake kuweza kukifikia;  hawezi kupata haki kwa njia ya Sheria.  "Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki [atakayefanywa kuwa mwenye haki] mbele zake kwa matendo ya sheria."  Ni hali ya kusikitisha jinsi gani!  Yatupasa kuwa na haki ya sheria ama sivyo hatuwezi kuingia mbinguni, walakini sheria hiyo haina haki ya kugawa hata kwa mmoja wetu.  Haitakubali kutugawia chembe ndogo mno ya utakatifu ambao pasipo huo hakuna mtu atakayemwona Bwana, hata kama sisi tutafanya juhudi zetu kwa ushupavu na nguvu.

     Ni nani, basi, awezaye kuokoka?  Je, yawezekana kuwa na kitu kama hicho cha kuwako mtu mwenye haki? ---- Ndio, kwa sababu Biblia mara kwa mara inazungumza juu ya watu kama hao.  Inazungumza juu ya Lutu kuwa "mtu huyu mwenye haki;" pia inasema,  "Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao" (Isa.3:l0), hivyo ni kuonyesha kwamba kutakuwako na watu wenye haki watakaopokea zawadi;  pia inatangaza kwa wazi kwamba litakuwako taifa lenye haki mwishoni,  inasema:  "Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda;  Sisi tunao mji ulio na nguvu;  Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma.  Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie."  Isa. 26:l,2.  Daudi asema,  "Na sheria yako ni kweli."  Zab.ll9:l42.  Hiyo [sheria] siyo kweli tu, bali ni jumla ya kweli yote;  basi, inafuata ya kwamba taifa lile lishikalo kweli litakuwa ni taifa lile lishikalo sheria ya Mungu.  Hao watakuwa ni watendaji wa mapenzi Yake, nao wataingia katika ufalme ule wa mbinguni.  Mt.7:2l.