>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Vielelezo hai vya ukombozi

Vielelezo hai vya ukombozi

VIELELEZO HAI VYA UKOMBOZI KUTOKA KATIKA UTUMWA

     Sasa hebu na tuchukue  baadhi ya vielelezo juu ya uwezo wa imani kuokoa kutoka  utumwani.  Tutadondoa Luka l3:l0-l7:-

     "Siku ya Sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo.  Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.  Yesu alipomwona alimwita, akamwambia,  Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.  Akaweka mikono yake  juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.  Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya Sabato, akajibu, akawaambia mkutano, kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.  Lakini   Bwana  akajibu akasema,  Enyi wanafiki,  Kila mmojawenu, je!  hamfungui ng'ombe wake au punda wake  siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha?  Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?  Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye;  mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na Yeye."

    Tunaweza kuachilia mbali mabishano ya mkuu huyo ili kuutafakari muujiza ule.  Mwanamke yule alikuwa amefungwa;  sisi nasi, kwa njia ya hofu ya mauti, tumekuwa katika hali ya utumwa maisha yetu yote.  Shetani alikuwa amemfunga mwanamke huyo;  Shetani pia ametega mitego kwenye miguu yetu, na kutuleta kifungoni.  Hakuweza kabisa kujinyosha;  maovu yetu yametushika hata hatuwezi kuinua macho  yetu na kutazama juu.  Zab.40:l2.  Kwa neno tu na mguso   Yesu alimweka huru mwanamke yule kutoka katika udhaifu wake;  hivi sasa tunaye Kuhani Mkuu yule yule mwenye rehema kule mbinguni, ambaye anachukuana nasi katika [anaguswa na] mambo yetu ya udhaifu, na neno lile lile litatuokoa toka maovuni.

     Ni kwa kusudi gani iliandikwa  miujiza hii ya uponyaji iliyofanywa na Yesu?  Yohana anatueleza.  Haikuwa tu kwa ajili ya kutuonyesha sisi kuwa anaweza kuponya magonjwa,   bali kuonyesha uweza wake juu ya dhambi.  Angalia Mt.9:2-8.  Lakini Yohana asema:-

    "Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki.  Lakini hizi zimeandikwa;  ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu;  na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake."  Yohana 20:30,3l.

     Basi tunaona ya kwamba hizo zimeandikwa tu kama vielelezo hai vya upendo wake Kristo, upendo wake wa kuwaondolea watu maumivu yao, na uweza wake wa kuziharibu kazi za  Shetani, haidhuru kama zimo mwilini au rohoni.  Muujiza mmoja zaidi utatosheleza tukiwa katika wazo hili.  Ni ule ulioandikwa  katika  kitabu cha Matendo ya Mitume sura ile ya tatu.  Sitadondoa kisa kile chote, bali namwomba msomaji kukifuatilia kwa makini katika Biblia yake.

     Petro na Yohana walipofika penye mlango ule wa hekalu walimwona mtu mmoja mwenye umri wa zaidi ya miaka arobaini, aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye.  Alikuwa hajapata kutembea kwa miguu yake.  Alikuwa akiomba, na Petro akajisikia anasukumwa na Roho kumpa mtu huyo kitu fulani kilicho bora kuliko fedha au dhahabu.  Akasema:  "Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.  Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.  Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda;  akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu." Fungu la 6-8.

     Muujiza huu maarufu juu ya mmoja ambaye wote walikuwa wamemwona ulisababisha mshangao miongoni  mwa watu;  naye Petro alipoona mshangao wao, akaanza kueleza jinsi muujiza huo ulivyofanyika:-

     "Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi?  Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi  mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe.  Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji;  mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu;  na sisi tu mashahidi wake.  NA KWA IMANI KATIKA JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU  mnayemwona na kumjua;  na imani ile iliyo kwake Yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote."  Mdo.3:l2-l6.

     Sasa tumia kielelezo hiki.    "Mtu huyu alikuwa kiwete toka tumboni mwa  mamaye," akiwa hana uwezo wa kujisaidia mwenyewe.  Angefurahi kuweza kutembea, lakini alikuwa hawezi kufanya hivyo.  Vile vile sisi sote tunaweza kusema pamoja na Daudi,  "Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu;  Mama yangu alinichukua mimba hatiani."  Zab.5l:5.  Matokeo yake, sisi kwa asili tu dhaifu sana hata hatuwezi kufanya mambo yale ambayo tungependa kufanya.  Kadiri kila mwaka wa maisha yake ulivyopita na kumwongezea kushindwa kwake kutembea, na kumwongezea uzito wa mwili wake, huku viungo vyake vikiwa havipati nguvu zaidi, ndivyo yalivyo mazoea ya kufanya dhambi tena na tena kadiri tunavyoendelea kukua na kuwa  wazee, yanaimarisha nguvu yake juu yetu.  Lilikuwa jambo lisilowezekana kabisa kwa mtu yule kutembea;  lakini jina lake Kristo, kwa imani katika jina hilo, lilimpa uzima mkamilifu na uhuru toka katika udhaifu wake.  Hivyo nasi, kwa njia ya imani katika Yeye, tunaweza kufanywa wazima, na kuwezeshwa kufanya kitu kile ambacho mpaka sasa kilikuwa hakiwezekani.  Kwa vile mambo yale yasiyowezekana kwa mwanadamu yanawezekana kwa Mungu.  Yeye ndiye Muumbaji.  "Humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo."  Mojawapo ya maajabu ya imani, kama ilivyodhihirishwa  katika watu wale  mashuhuri wa kale, ni kwamba "walitiwa  nguvu baada ya kuwa dhaifu."

     Kwa mifano hii tumeona jinsi Mungu anavyookoa kutoka utumwani wale wanaomtumaini.  Sasa hebu na tutafakari  maarifa ya kuudumisha uhuru huo.

     Tumekwisha kuona ya kwamba sisi kwa asili ni watumwa wa dhambi na Shetani,  na  ya kwamba mara tu sisi tunapojitoa nafsi zetu kwake Kristo, tunafunguliwa toka katika nguvu yake Shetani.  Asema Paulo:  "Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki."  Rum.6:l6.  Basi, mara tu sisi tunapokuwa huru kutoka katika utumwa wa dhambi, tunakuwa watumwa wake Kristo.  Naam, tendo lile la kutufungua kutoka katika nguvu ya dhambi, kama jibu kwa imani yetu, huthibitisha kukubalika kwetu na Mungu kama watumishi wake.  Naam, tunakuwa watumwa wake Kristo kwa mkataba;  lakini, yule ambaye ni mtumwa wa Bwana ni mtu huru, maana sisi tumeitwa tupate uhuru (Gal.5:l3),  walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru (2 Kor.3:l7).

     Sasa pambano linakuja tena.  Shetani hana tabia ya kumwachilia mtumwa wake kwa urahisi.  Anakuja,  akiwa amevaa silaha ya kiboko cha jaribu kali, kutuswaga sisi tena katika utumishi wake.  Kwa masikitiko tunajua kwamba yeye ana nguvu kuliko sisi, na ya kwamba bila kusaidiwa hatuwezi kumpinga.  Lakini tunaogofywa na nguvu yake, nasi tunalia ili kuomba msaada.  Hapo ndipo tunapokumbuka ya kwamba sisi sio watumwa tena wa Shetani. Tulijitoa nafsi zetu kwa Mungu, na kwa sababu hiyo alitukubali  sisi kama watumwa WAKE.  Basi, tunaweza kusema pamoja na Mtunga Zaburi,  "Ee BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako, Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako, Umevifungua vifungo vyangu."  Zaab.ll6:l6.  Lakini ukweli ni kwamba Mungu amevifungua vifungo ambavyo Shetani alikuwa ametufunga navyo  ----  naye amefanya hivyo kama tukiamini kwamba amefanya  hivyo  ----  ni ushuhuda kwamba Mungu atatulinda, kwa maana anawatunza  hao walio wake, nasi tunayo hakika kwamba Yeye aliyeanza kazi  njema ndani yetu "ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu."  Wafilipi l:6.  Na katika tumaini hili tunapata nguvu ya kumpinga [Shetani].

     Tena, kama sisi tumejitoa nafsi zetu wenyewe kuwa watumishi wa Mungu, basi, sisi ni  watumishi Wake, au, kwa maneno mengine, sisi ni silaha za haki mikononi mwake.  Soma Rum.6:l3-l6.  Sisi sio silaha zilizokufa, zisizokuwa na uhai, zisizokuwa na akili, kama zile  anazozitumia bwana shamba, ambazo hazina sauti ya kusema jinsi zinavyotaka zitumike, bali ni silaha  zilizo hai, zenye akili, ambazo zinaruhusiwa kuchagua kazi yao.  Hata hivyo, neno hili "silaha"  humaanisha chombo,  ----  kitu ambacho kiko chini ya udhibiti wa mfanya kazi.  Tofauti kati yetu na vyombo vya fundi mashine ni kwamba sisi tunaweza kuchagua nani atutumie, na kwa kazi gani tutatumika;  lakini baada ya kufanya uchaguzi huo, na kujikabidhi wenyewe mikononi mwa mfanya kazi huyo,  inatupasa kuwa mikononi mwake kikamilifu kama chombo kinavyokuwa, ambacho chenyewe hakina sauti ya kusema kitakavyotumika.  Tunapojitoa nafsi zetu kwa Mungu, inatupasa kuwa mikononi  mwake kama vile udongo wa  mfinyanzi ulivyo mikononi mwa mfinyanzi, ili apate kutufanya sisi kama apendavyo.  Uchaguzi wetu wa hiari unakuwa katika kuchagua kama tutamruhusu au hatutamruhusu kufanya kazi ile iliyo njema ndani yetu .

     Wazo hili la kuwa silaha mikononi mwa Mungu, kama likizingatiwa kikamilifu, ni msaada wa ajabu katika kujipatia ushindi ule wa imani.  Kwa maana, angalia, kile silaha hiyo itakachoweza kufanya  hutegemea kabisa  juu ya mtu yule ambaye silaha hiyo imo mkononi mwake.  Hapa, kwa mfano, ni dadu.  Yenyewe haina ubaya wo wote, lakini inaweza kutumika kwa makusudi mabaya mno, kama inavyoweza kutumika kwa manufaa mazuri.  Kama imeangukia mikononi mwa mtu mwovu,  inaweza kutumika kutengenezea sarafu ya bandia.  Bila shaka haitatumika kwa kusudi lo lote jema.  Lakini ikiangukia mikononi mwa mtu mnyofu, safi,  huenda isilete madhara yo yote.  Vivyo hivyo, sisi tulipokuwa watumwa wa Shetani, hatukufanya jema  lo lote (Rum.6:20);  lakini sasa tukiwa tumejitoa nafsi zetu mikononi mwa Mungu, tunajua  kwamba hakuna udhalimu wo wote ndani yake, basi, silaha hii ikiwa mkononi mwake haiwezi kutumiwa kwa kusudi baya.  Kule kujitoa nafsi zetu kwa Mungu lazima kuwe kwa ukamilifu ule ule kama kulivyokuwa tulipojitoa kwa Shetani,  kwa maana mtume asema hivi:-

     "Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu.  Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa."  Rum.6:l9.

     Hivyo, siri yote ya ushindi hutegemea kwanza katika kujitoa kabisa kwa Mungu, pamoja na kuwa na tamaa ya kweli ya kufanya mapenzi Yake;  pili, kujua kwamba katika kujitoa nafsi zetu kwake, Yeye anatukubali sisi kama watumishi Wake;  kisha, kuendelea  kujitoa hivyo kwake, na kujiweka mikononi mwake.  Mara nyingi ushindi huu unaweza kupatikana tu kwa kurudia tena na tena kusema, "EE BWANA, HAKIKA MIMI NI MTUMISHI WAKO;  Mtumishi wako,  Mwana wa mjakazi  wako;  UMEVIFUNGUA VIFUNGO VYANGU."   Hii ni njia ya kusisitiza tu kusema, "Ee Bwana, nimejitoa nafsi yangu mikononi mwako kama silaha ya haki;  mapenzi yako na yatimizwe, wala sio ile amri ya mwili wangu."  Lakini hapo tunapoweza kutambua nguvu ya andiko hilo na kujisikia  ya kwamba sisi ni watumishi wa Mungu, basi litatujia mara moja wazo hili,  "Naam, kama mimi kweli ni silaha mikononi mwa Mungu, basi, hawezi kunitumia mimi kufanya maovu, wala hawezi kuniruhusu mimi kufanya maovu kwa kadiri ninavyodumu kuwa mikononi mwake.  Iwapo mimi nitalindwa na maovu, basi, ni lazima atanilinda mimi, kwa sababu mimi siwezi kujilinda mwenyewe.  Walakini Yeye anataka kunilinda mimi kutoka maovuni, maana ameonyesha hamu yake hiyo, na pia  uweza wake kutimiza hamu yake hiyo, kwa kujitoa nafsi yake kwa ajili yangu.  Kwa hiyo,  mimi nitalindwa na maovu."  Mawazo yote hayo yanaweza kupita kichwani kwa ghafula;  pamoja nayo  lazima itakuja hisia ya furaha kwamba sisi tutalindwa kutoka katika uovu huo wa kuchukiza.  Furaha hiyo kwa kawaida hujitokeza katika shukrani kwa Mungu, na wakati tunapomshukuru Mungu adui hurudishwa nyuma pamoja na jaribu lake, na amani ya Mungu hujaa moyoni.  Hapo ndipo tunapotambua kwamba furaha inayotokana na kuamini inapita furaha yote inayopatikana kwa kujifurahisha  katika dhambi.

     Yote haya  ni uthibitisho wa maneno ya Paulo:  "Basi, je! twaibatilisha sheria kwa imani hiyo?  Hasha!  kinyume cha hayo twaithibitisha sheria."  Rum.3:3l.  Kule ku"ibatilisha sheria"  sio kuifuta;  maana hakuna mwanadamu awezaye kuifuta sheria  ya Mungu, walakini  Mtunga Zaburi anasema kwamba imetanguliwa.  Zab.ll9:l26.  Kuitangua sheria ya Mungu ni zaidi ya kudai kwamba haina maana yo yote;  ni kuonyesha kwa  njia ya maisha yetu kuwa haina maana yo yote.  Mwanadamu anaibatilisha sheria ya Mungu anapokiri kuwa haina uwezo wo wote katika maisha yake.  Kwa kifupi,   kuibatilisha sheria ni kuivunja;  lakini sheria yenyewe inabaki  jinsi ilivyo  bila kujali kama inashikwa au la.  Kuibatilisha kunamwathiri tu mtu mwenyewe.

     Kwa hiyo, mtume anaposema kwamba hatuibatilishi sheria ya  Mungu kwa imani, bali, kinyume chake, tunaithibitisha, anamaanisha kwamba haituongozi kuivunja sheria hiyo, bali kuitii.  La,  tusingesema ya kwamba imani  INATUONGOZA kutii, bali kwamba imani yenyewe inatii.  Imani inaithibitisha sheria moyoni.  "Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo."  Kama jambo litarajiwalo ni haki, basi, imani inaithibitisha.  Badala ya imani hii kuongoza kwenye imani ile isemayo kwamba katika kipindi hiki cha Injili sheria haina maana yo yote kwa Mkristo kwa sababu imani peke yake ndiyo ya muhimu kwa wokovu, imani hii ndiyo peke yake iko kinyume na wale wanaopinga sheria na kuitukuza imani.  Haidhuru mtu ajisifu kiasi gani kuwa anaishika sheria ya Mungu, kama anakana au anaipuza imani hii kamili katika Kristo, hali yake sio bora kuliko ile ya mtu yule anayeishambulia moja kwa moja sheria hiyo.  Mtu aliye na imani huyo ndiye peke yake anayeiheshimu kweli kweli sheria ya Mungu.  Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu (Ebr.ll:6);  pamoja na hiyo, yote yawezekana (Marko 9:23).

     Ndio, imani inafanya yale yasiyowezekana,  na ni jambo lilo  hilo analotutaka Mungu tulifanye.  Yoshua aliposema kwa Israeli,  "Hamwezi kumtumikia Bwana,"  ilikuwa ni kweli kwamba Mungu aliwataka kumtumikia.  Haimo katika uwezo wa mtu ye yote kutenda haki, hata kama anataka kufanya hivyo (Gal.5:l7);  kwa hiyo ni kosa kusema kwamba yote anayotaka Mungu kwetu ni kufanya vizuri sana  kwa kadiri tuwezavyo.  Yule ambaye hafanyi zaidi ya hapo hataweza kuzifanya kazi zake Mungu.  La, ni lazima AFANYE ZAIDI KULIKO VILE AWEZAVYO KUFANYA.  Ni lazima afanye  kile ambacho ni nguvu ya Mungu peke yake,  ikifanya kazi ndani yake,  inamwezesha kufanya.  Haiwezekani kwa mwanadamu kutembea juu ya maji, lakini Petro alifanya hivyo alipotumia imani katika Yesu.

     Kwa kuwa mamlaka yote mbinguni na duniani yamo mikononi mwake Kristo, na nguvu hiyo iko tayari kwa ajili yetu, na Kristo Mwenyewe anakuja kukaa moyoni mwetu kwa imani, basi, hakuna nafasi ya kumlaumu Mungu kwa kututaka sisi kufanya yale yasiyowezekana;  maana  "Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu."  Luka l8:27.  Kwa hiyo, kwa ujasiri kabisa tunaweza kusema,  "Bwana  ndiye  anisaidiaye, sitaogopa;  Mwanadamu atanitenda nini?"  Ebr.l3:6.  Kisha tutasema,  "Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo?  Je! ni dhiki, au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?"   ----  "Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa Yeye aliyetupenda."  Rum.8:35,37.  "Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala  yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine cho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu."