>Mwanzo >Soma vitabu >Tokeni Mijini >Tokeni Mijini: Dibaji

Tokeni Mijini: Dibaji

Dibaji

 Faida za kuishi shamba [vijijini] zimesisitizwa tena na tena katika mashauri yanayotolewa na Roho ya Unabii. Mawingu ya dhoruba yanayojikusanya yanaashiria kwamba yafaa kuanza kupaza sauti ili kutoa wito wa kuihama miji. Ni budi iwe wazi kwa kila Mwadventista Msabato mwenye akili kujua ya kwamba kuishi mjini, pamoja na msongamano wa watu uliopo, vishawishi vyake na migogoro ya vyama vya wafanyakazi inayozidi kuongezeka, hakuweki mazingira yenye kuleta afya kwa familia za Kikristo.

 Kwa miaka mingi maelfu ya Waadventista Wasabato wameelekezwa kuchagua mazingira yanayofaa kuweka makazi yao na katika uhusiano wao na mashirika ya ulimwengu kwa njia ya mashauri yatokanayo na shuhuda juu ya mambo hayo ya maana sana ambayo yamechapishwa na kutawanywa katika sehemu nyingi. Ishara mbaya za hatari kubwa iliyo karibu sana kutokea zinapoonyesha ugumu wa kuzitambua hatari hizo na ukali mno wa pambano lililo mbele yetu, inaonekana kwetu ya kwamba ni jambo linalofaa kuuchapisha tena ushauri huu kwa kutumia mtindo huu ambao unaweza kuyanasa mawazo ya kila mshiriki wa kanisa.

 Na kwa kufikiria nyakati hizi tulizo nazo [hivi sasa], ni mahali pake, sio tu kurudia ushauri ule unaofahamika sana uliochapishwa muda mrefu uliopita, bali kuzitilia nguvu semi hizo kwa kuzitoa kwa mafundisho ya kinagaubaga yaliyopata kuchapishwa toka wakati hata wakati katika gazeti la Review and Herald au yaliyoandikwa katika barua zake za ushauri zilizoandikwa kwa watenda kazi waliokabidhiwa madaraka katika kazi ya Mungu. Kitendo kama hicho kinapatana kabisa na maagizo ya Bibi E. G. White kwa wadhamini wake ili waweze kutayarisha "kwa ajili ya kuchapishwa maandiko yangu yaliyokusanywa pamoja kutoka katika maandiko yangu ya mkono," kwa maana, kama alivyosema yeye mwenyewe yana "maagizo aliyonipa Bwana kwa ajili ya watu wake." Mwaka wa kuandikwa au kuchapishwa kwa mara ya kwanza umetolewa pamoja na kumbukumbu ya chanzo cha kila kifungu cha maneno [kilichotumika].

 Wito wa dhati uliotolewa katika kijitabu hiki unataka pawepo na nia ya kutekeleza jambo hili, lakini [kwa wakati uo huo] onyo hili zito linatolewa ili watu wetu wasithubutu kukurupuka [kufanya mambo bila kufikiri na kupanga vizuri]. Tungependa kuyaelekeza mawazo yenu hasa kwa tahadhari zile zinazopatikana katika Sehemu ya Saba, "Kuongozwa kwa Maongozi ya Mungu," ambayo inatokea kwenye kurasa za . Kijitabu hiki sasa kinawekwa uwanjani kama jibu la msimamo ulioamuliwa na viongozi wa kanisa hili kwamba [sasa] wakati umefika wa kurudia kusema tena na tena kilio kile cha, "TOKENI MIJINI."

 

            WADHAMINI WA UCHAPISHAJI WA MAANDIKO YA ELLEN G. WHITE