>Mwanzo >Soma vitabu >Tokeni Mijini >Tokeni Mijini: Sehemu ya Sita

Tokeni Mijini: Sehemu ya Sita

SURA YA SITA

 

Tusikae Wengi Mahali Pamoja Katika Vituo Vya Taasisi Zetu

 

Tusikae Wengi Mahali Pamoja

 Katika siku zetu hizi Bwana anataka watu wake watawanyike ulimwenguni kote. Haiwapasi kukaa wengi mahali pamoja. Yesu alisema, "Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe [mtu]." Marko 16:15. Wanafunzi walipofuata mapenzi [matakwa] yao ya kubaki kwa idadi kubwa kule Yerusalemu, mateso yaliruhusiwa kuwapata, nao wakatawanyika kwenda mahali pote katika ulimwengu ule uliokaliwa na watu.

 Kwa miaka mingi ujumbe huu wa onyo na wa kuwasihi umekuwa ukija kwa watu wetu, ukiwashurutisha kusonga mbele na kuingia katika shamba la Bwana la mavuno, na kufanya kazi bila kujifikiria wenyewe kwa ajili ya roho za watu. ----- Testimonies, Gombo la 8, uk 215. (1904)

Tawanyikeni Na Kwenda Kule Wasikolipata Onyo Hilo

 Washiriki wa makanisa yetu makubwa ni wengi ambao karibu hawafanyi kitu cho chote kabisa. Hao wangeweza kufanikiwa kufanya kazi nzuri kama wangeweza kutawanyika na kwenda mahali ambako kweli hii bado haijaingia badala ya kujikusanya wengi mahali pamoja. Miti iliyopandwa karibu karibu sana haisitawi. Hupandikizwa mahali pengine na mwenye bustani ili ipate nafasi ya kutosha kukua, isizuiwe kukua zaidi wala isiwe dhaifu. Kanuni iyo hiyo ingefanya kazi yake vizuri kwa makanisa yetu makubwa. Wengi miongoni mwa washiriki wetu wanakufa kiroho kwa kukosa kazi hii hii [ya kwenda mahali kule ambako ujumbe bado haujafika]. Wanakuwa dhaifu, tena wanashindwa kufanya kazi yao vizuri. Wangepandikizwa [wangehamia] mahali pengine, wangeweza kupata nafasi ya kutosha kuweza kukua [kiroho] na kuwa na nguvu.

 Si kusudi lake Mungu kwamba watu wake wakae wengi mahali pamoja, au waishi pamoja katika jumuia kubwa. Wanafunzi wa Yesu ni wawakilishi wake hapa duniani, na Mungu anakusudia kwamba wao watatawanyika kila mahali duniani, katika miji midogo, miji mikubwa, na vijijini, na kuwa kama mianga kati ya giza nene la ulimwengu huu. Wanapaswa kuwa wamishonari wa Mungu, kwa imani yao wakishuhudia ukaribu sana wa marejeo ya Mwokozi wao.

MAHALI PALE ILIPOFUNGUKA NJIA YA KUJIPATIA RIZIKI

 Washiriki walei [wa kawaida] wa makanisa yetu wanaweza kufanikiwa kufanya kazi ile ambayo, hata sasa, hawajaanza kuifanya. Wasiwepo watu wanaohamia mahali papya kwa ajili ya faida ya kidunia tu; bali mahali pale ilipofunguka njia ya kujipatia riziki ziende familia zile zilizojizatiti katika kweli, familia moja au mbili hivi ziende mahali pamoja kufanya kazi kama wamishonari. Wangejisikia kuwa wanayo haja ya kuwapenda watu, kwamba wanao mzigo wa kuwashughulikia watu hao, tena, kama somo lao, wangejifunza namna ya kuwaingiza katika kweli hii. Wanaweza kugawa vitabu vyetu, kufanya mikutano nyumbani mwao, kufahamiana na majirani zao, na kuwaalika waje kwenye mikutano hiyo. Wanaweza kuiacha nuru yao kuangaza kwa matendo yao mema. ----- Testimonies, Gombo la 8, uk. 244,245. (1904)

Vishawishi Vya Taasisi Zetu Visiwavute

 Wale wanaojisikia kupenda kuishi karibu na nyumba yetu ya kuchapisha vitabu au hospitali na shule yetu iliyo kwenye bustani ile kubwa ya Takoma [Takoma Park] hawana budi kupata ushauri kabla hawajahamia huko

 Kwa wale wanaotarajia kwenda kule Mountain View kama ndipo mahali pazuri pa kuishi, ati kwa sababu tu mtambo wetu wa kuchapisha vitabu wa Pasifiki [Pacific Press] utajengwa pale, ningependa kuwaasa hivi: Zitupieni macho sehemu nyingine za ulimwengu zinazohitaji nuru yenu mliyoipokea kama amana. Kumbukeni kwamba Mungu amempa kila mtu kazi yake. Chagueni mahali fulani mtakapokuwa na nafasi nzuri ya kuiacha nuru yenu kuangaza kati ya giza hilo la kimaadili.

 Inatokea sikuzote ya kwamba taasisi yetu inapojengwa mahali fulani, ziko familia nyingi zinazotaka kwenda huko na kuweka makao yao karibu nayo. Hivyo ndivyo ilivyokwisha kutokea kule Battle Creek na Oakland, na, kwa kiwango fulani, karibu kila mahali ambapo tunayo shule au hospitali yetu. ----- Fundamentals of Christian Education, uk. 494,495. (1904).

Msianzishe Vituo Vya Yerusalemu

 Watu wetu ... hawapaswi kupaangalia ... kama kituo cha Yerusalemu. Wasifikiri kwamba kwa sababu idadi fulani ya ndugu zetu wameitwa kuja hapa kujiunga na kazi hii ya uchapishaji, basi, hapa ndipo mahali pa kukaa idadi kubwa ya watu wetu na familia zao. Na kila mtu anayehusika na Ofisi hiyo ajiweke tayari kuondoka endapo Mungu atamwita kwenda mahali fulani papya. ----- Manuscript 148, 1905.

 Msisongamane mahali pamoja, mkifanya kosa lile lile lililokwisha kufanywa kule Battle Creek. Kuna mamia ya mahali pengine panapohitaji nuru hiyo aliyowapa Mungu. ----- Fundamentals of Christian Education, uk. 495. (1904).

Bakini Katika Makanisa Madogo - Anzisheni Shule Nyingi Mpya

 Familia nyingi ambazo, kwa madhumuni ya kuwapatia elimu watoto wao, huhamia mahali kule zilikojengwa shule zetu kubwa, wangeweza kufanya kazi bora kwa ajili ya Bwana kwa kuendelea kubaki pale pale walipo. Wangelitia moyo kanisa ambalo wao ndio washiriki wake kujenga shule ya kanisa ambayo watoto walio katika mipaka yake wangeweza kujipatia elimu kamili ya Kikristo itakayowawezesha kufanya kazi yao. Lingekuwa ni jambo bora sana kwa watoto wao, kwao wenyewe, na kwa kazi ya Mungu, kama wangeendelea kubaki katika makanisa hayo madogo, ambamo msaada wao unahitajika badala ya kwenda kule yaliko makanisa yetu makubwa, ambako, kwa vile wao hawahitajiki [hawatakuwa na kazi kanisani], kuna majaribu daima ya kuanguka katika uzembe [uvivu] wa kiroho.

 Po pote pale walipo Wasabato wachache, wazazi wangeungana pamoja na kutenga eneo kwa ajili ya shule ya kutwa ambamo watoto na vijana wao wanaweza kupata mafunzo yao. Wamwajiri mwalimu Mkristo, ambaye, kama mmishonari aliyejitoa wakf, ataweza kuwaelimisha watoto wao kwa njia ambayo itawafanya nao wawe wamishionari. ----- Counsels to Teachers, uk. 173,174. (1913)

Hivi Malaika Wanajisikiaje

 Nafikiria jinsi malaika wanavyojisikia wanapouona mwisho ule ukikaribia, na kuwaona wale wanaodai kuwa wanayo maarifa ya kumjua Mungu na Yesu Kristo aliyemtuma, wakisongamana sana mahali pamoja, wakikaa wengi mahali pamoja, na kuhudhuria mikutano yao, na kuwa na hisia ya kukata tamaa na kutoridhika endapo hakuna mahubiri mengi yanayozinufaisha roho zao na kuliimarisha kanisa, wakati wao hawafanyi kazi yo yote kabisa. ----- Letter 16e, 1892.

Ipanueni Kazi na Kuieneza - Ila Sio Pale Makao Makuu

 Watu wanahamasishwa [wanatiwa moyo] kulundikana pale Battle Creek, tena wanalipa zaka yao na kutoa mvuto wao ili ipate kujengwa Yerusalemu ya leo pale ambayo haifuati mpango wa Mungu. Kwa kufanya kazi hiyo mahali pengine panakosa msaada ambao wangeweza kuupata. Panueni kazi, enezeni, naam; lakini sio mahali pamoja. Tokeni na kujenga vituo vyenye mvuto mahali pale ambapo hakuna kitu au karibu hakuna cho chote kilichofanyika pale. Livunje-vunjeni kundi hilo kubwa sana lililosongamana mahali pamoja; tawanyeni miali ya nuru ile iokoayo, na kuiangaza nuru hiyo katika pembe [kona] za dunia zilizotiwa giza. ----- Testimonies to Ministers, Uk. 254,255. (1895)