SEHEMU YA SABA
Kuongozwa na Maongozi ya Mungu
Mungu Anapoifungua Njia
Wakati umefika, ambapo, kadiri Mungu anavyoifungua njia, familia hazina budi kutoka mijini. Watoto wapelekwe kule shamba [vijijini]. Wazazi na wajipatie mahali panapofaa kulingana na fedha walizo nazo zitakavyoruhusu. Ingawa nyumba ile iliyojengwa inaweza kuwa ndogo, hata hivyo, pangekuwapo na shamba linaloweza kulimwa kuambatana nayo. ----- Manuscript 50, 1903.
Mungu Atawasaidia Watu Wake
Wazazi wanaweza kujijengea nyumba ndogo huko shamba [vijijini], na kuwa na mashamba ya kulima, ambamo wanaweza kuwa na viunga vya miti ya matunda, na kupanda mboga za majani pamoja na matunda madogodogo ili kuchukua mahali pa nyama, ambayo inaichafua sana damu inayopita katika mishipa na kuleta uzima. Mahali hapo watoto hawatazungukwa na mivuto ile miovu ipatikanayo katika maisha yale ya mjini. Mungu atawasaidia watu wake kupata makazi kama hayo nje ya miji [wakimwomba]. ----- Medical Ministry, uk. 310. (1902)
Kusaidia Kuifungua Njia
Wakati unapozidi kusonga mbele, watu wetu wengi zaidi na zaidi watalazimika kuihama miji. Kwa miaka mingi tumeagizwa ya kwamba ndugu na dada zetu, na hasa familia zile zenye watoto, wangefanya mpango wa kuondoka mijini kwa kadiri njia inavyofunguka mbele yao na kuwawezesha kufanya hivyo. Wengi watalazimika kufanya kazi ngumu kwa bidii ili kusaidia kuifungua njia. Lakini mpaka hapo itakapowezekana kwao kuhama, kadiri wanavyoendelea kubaki humo, wangefanya bidii kubwa sana kufanya kazi ya umishonari, haidhuru eneo la mvuto wao liwe dogo jinsi gani. ----- Review and Herald, Sept. 27, 1906.
Ushauri na Onyo Kwa Wale Wanaotarajia Kuondoka Mijini
[Barua hii iliandikwa Desemba 22, 1893, kuijibu barua iliyotoka kwa kiongozi maarufu wa Battle Creek, akimjulisha Bibi White kuwa kama itikio lao kwa onyo lile linalowataka watu wetu kuhama kutoka Battle Creek, "kati ya watu mia moja na mia mbili" hivi walikuwa wanajiandaa kuondoka "kwa haraka iwezekanavyo." ----- WAKUSANYAJI WA MAANDIKO.]
Ndugu yangu, barua yako inaniambia kwamba wapo wengi waliopata mwamko mkubwa wa kuondoka Battle Creek. Ipo haja, haja kubwa, ya kazi hiyo kufanyika, na kufanyika sasa. Wale wanaojisikia kuhama hivi mwishoni hebu isiwe kwa kukurupuka, kwa msisimko, au bila kufikiri, au kwa njia ambayo hatimaye watajuta sana kuhama kwao....
Angalieni sana pasiwepo na kuhama kunakofanywa bila kufikiri katika kulitii onyo hilo la kuhama kutoka Battle Creek. Msifanye jambo lo lote bila kuitafuta hekima toka kwa Mungu, ambaye ameahidi kuwapa kwa ukarimu wale wote wamwombao, na ambaye hakemei [Yakobo 1:5]. Yale yote ambayo mtu ye yote anaweza kufanya ni kuwapasha habari tu na kutoa ushauri wake, kisha kuwaacha wale wanaoamini kwa dhati kuhusu wajibu wao wa kuhama, wakiwa chini ya uongozi wake Mungu, kufanya hivyo; mioyo yao yote ikiwa imefunguliwa wazi ili wapate kujifunza na kumtii Mungu.
Mimi nasumbuka sana moyoni mwangu kufikiri kwamba huenda wapo hata baadhi ya waalimu [wachungaji, n.k.] wetu ambao wanahitaji kuwa na busara zaidi ili waweze kufikiria pande zote [za jambo hilo]. Wajumbe wale wanaouchukua ujumbe huo wa rehema kwa ulimwengu wetu, ambao wanategemewa na watu wetu, wataombwa kutoa mawaidha [maoni] yao. Tahadhari kubwa haina budi kutumika kwa upande wa watu hao ambao hawana uzoefu halisi wa maisha ya kujitegemea [vijijini] kwa kufanya kazi [kwa mikono yao], na ambao watakuwa hatarini kutoa mawaidha yao, wasijue mawaidha yao hayo yatasababisha watu wengine kufanya kitu gani.
KIPAWA CHA KUTOA USHAURI
Watu wengine wanaona mbali katika mambo mengi, hao wanao uwezo wa kutoa ushauri. Ni kipawa cha Mungu. Katika nyakati zile ambazo kazi ya Mungu inahitaji maneno ya busara na ya dhati, na yale yaliyo thabiti, hao wanaweza kusema maneno fulani ambayo yatawafanya watu wale waliochanganyikiwa pamoja na wale walio gizani [wasioelewa kitu], kuiona kwa ghafula, kama vile nuru ya mwanga wa jua inavyomulika ghafula, njia ile wanayopaswa kuifuata katika jambo lile lililowajaza mashaka mengi na kuifadhaisha sana mioyo yao wakati walipokuwa wakifanya uchunguzi wao uliowachukua majuma mengi na miezi mingi. Ufumbuzi upo, yaani, ufyekaji wa njia ile iliyo mbele yao, na Mungu ameruhusu mwanga wake wa jua kuingia mawazoni mwao, nao wanaona ya kuwa maombi yao yamejibiwa, yaani, njia yao iko wazi. Lakini basi, mawaidha fulani yanaweza kutolewa bila kufikiri, yakisema ----- tokeni tu Battle Creek, wakati hakuna maelezo yo yote yaliyofafanuliwa vizuri kuhusu maendeleo gani watakayofanya katika maisha yao ya kiroho kwa ajili yao wenyewe au kwa ajili ya wengine kwa kuichukua hatua hiyo [ya kuhama].
FIKIRIENI KWA MAKINI SANA KILA HATUA YA KUHAMA KWENU
Hebu kila mmoja awe na muda wa kutosha wa kufikiria [jambo hilo] kwa makini [uangalifu] sana; asije akafanana na mtu yule aliyetajwa katika mfano [wa Yesu] aliyeanza kujenga, kisha akashindwa kumaliza. Kuhama ko kote kusifanyike isipokuwa kama kuhama huko na matokeo yake yote yamefikiriwa kwa makini sana ----- yaani, kila jambo limepimwa kuona uzito wake... Kwa kila mtu kazi ilitolewa kulingana na uwezo wake. Basi, asihame akiwa na mashaka, bali ajizatiti, na wakati uo huo akiwa ananyenyekea kwa kumtegemea Mungu.
Huenda wakawapo watu ambao watataka kuharakisha kufanya jambo fulani, na kujiingiza katika shughuli fulani ambayo hawaijui kabisa. Mambo hayo Mungu hataki. Fikiri kwa moyo mnyofu, kwa maombi, ukijifunza Neno [la Mungu] kwa makini sana na kwa maombi, akili yako na moyo wako vikiwa tayari kuisikiliza sauti ya Mungu.... Kuyajua mapenzi ya Mungu [katika suala hili] ni jambo kubwa.
MIPANGO ILIYOPANGWA VIZURI INATAKIWA
Nayatoa maneno haya kwa kanisa lile lililoko kule Battle Creek ili lipate kutembea katika mashauri ya Mungu. Haja ipo ya kuhama kwenu ----- yaani, wengi wenu kuhama kutoka Battle Creek ----- tena, ipo haja pia ya ninyi kuwa na mipango iliyopangwa vizuri juu ya kile mtakachofanya mtakapohama toka Battle Creek. Msiende kwa kukimbia, bila kujua mnachofanya.... Laiti kama wangekuwapo majenerali wenye hekima, wanaowafikiria wengine, watu wale wanaoyachunguza mambo kwa kuangalia kila upande, watakaokuwa washauri salama, ambao kidogo wanajua kile kilichomo ndani ya mwanadamu, wale ambao wanajua kuongoza na kushauri katika kicho chake Bwana.
HATARI INAAMBATANA NA UZOEFU MPYA
Nimekwisha kuona kwamba hatari inaambatana na kila awamu mpya ya uzoefu kanisani, kwa sababu wengine wanayasikia mambo hayo kwa moyo wenye kusisimka sana. Wakati waalimu [wachungaji, n.k.] wengine wanaweza kuwa imara upande ule wa kufundisha mafundisho ya Biblia, si wote watakaokuwa wamepata uzoefu wa maisha ya kujitegemea, si wote watakaowashauri wale waliochanganyikiwa kwa hakika na usalama. Hawaitambui hali hiyo ya kutatanisha ambayo haina budi kuja kwa kila familia itakayofanya mabadiliko hayo. Kwa hiyo, wote wawe waangalifu sana kuchunga maneno yao wanayosema; kama hawayajui mawazo ya Mungu katika baadhi ya mambo, basi, wasiseme kabisa kwa kukisia-kisia tu au kwa kudhani kuwa mambo hayo yako hivyo. Kama hawajui kitu cho chote kilicho dhahiri, hebu na waseme hivyo, na kuwaacha watu kila mmoja peke yake wapate kumtegemea Mungu. Hebu maombi mengi yafanyike, hata kwa kufunga, ili mtu ye yote asije akahama akiwa gizani [hajui la kufanya], bali ahame akiwa nuruni [anajua la kufanya] kama vile Mungu alivyo nuruni....
HAMENI KWA HADHARI
Hebu pasiwepo na kitu cho chote kinachofanywa bila utaratibu, isije ikatokea hasara kubwa au kupoteza mali kwa sababu ya hotuba motomoto zilizotolewa zenye kujaa misisimko ndani yake ambazo zinaamsha shauku ambayo haimo katika mpangilio wa Mungu, hata ushindi ule uliokuwa wa lazima kupatikana uweze kugeuka na kuwa kushindwa kunakotokana na kukosa utulivu wa kusimamia mambo vizuri na kuyafikiria vizuri, na kujenga juu ya kanuni na makusudi yaliyo imara. Hebu na pawepo na uongozi wa busara katika jambo hilo, na wote wapate kuhama chini ya uongozi ule wenye hekima wa Mshauri yule asiyeonekana, ambaye ni Mungu. Mambo ya kibinadamu yatajitahidi kutawala, na huenda pakawa na kazi iliyofanyika ambayo haina sahihi [idhini] ya Mungu. Basi, namsihi kila mtu asiwaangalie washiriki hao wa kibinadamu kwa nia na imani thabiti sana, bali amwangalie kwa bidii nyingi sana Mungu, mshauri mmoja aliye a hekima. Wekeni njia zenu zote na mapenzi [nia] yenu ili yapatane na njia za Mungu na mapenzi yake....
MATOKEO YA HATUA ZA HARARA
Endapo wengine watahama kwa haraka na kukimbia toka Battle Creek, halafu wakajikuta wameingia katika hali ya kukata tamaa, basi, watatoa shutuma zao, sio juu yao wenyewe, kwa kuhama kwao bila kutumia busara, bali juu wa wengine, ambao watawalaumu kuwa walitia shinikizo lao juu yao [mpaka wakawa wamehama]. Kutibuliwa kwa mipango yao yote na kushindwa kwao kutawafanya wawarudishie shutuma zote wale ambao wasingestahili kupewa sifa mbaya kama hizo....
Sasa, hivi sasa, ndio wakati ambao hatari zile kubwa za siku za mwisho zinazidi kuongezeka sana kutuzunguka pande zote, tunahitaji watu wenye hekima kuwa washauri wetu, sio watu wale watakaoona kwamba ni wajibu wao kuwasisimua watu na kuleta machafuko, bali ni wale wawezao kutoa mashauri yao ya busara na kuratibu na kupanga mipango ili kwamba kila msisimko unaotokea upate kuleta mpangilio mzuri kutoka katika machafuko yaliyopo, na kuleta raha na amani kwa njia ya kulitii Neno la Bwana. Hebu kila mtu na apatikane mahali pake panapomfaa hasa, ili apate kumfanyia Mungu kazi fulani, kulingana na uwezo wake aliopewa....
Kwa jinsi gani jambo hilo litaweza kufanyika? "Jitieni nira yangu," asema Yesu Kristo, yule aliyewanunua ninyi kwa damu yake ya thamani, ninyi ambao ni watumishi na mali yake, "mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi." Endapo kila mmoja atakuja kwa Yesu akiwa na moyo ulio tayari kufundishwa, moyo wenye toba, hapo ndipo atakuwa katika hali ya kiakili ya kuweza kufundishwa na kujifunza kwa Yesu na kuyatii maagizo yake....
WEKENI KILA MPANGO MLIO NAO MBELE ZAKE MUNGU
Hatuwezi kuwa na imani dhaifu sasa; hatuwezi kuwa salama kwa kuwa na mtazamo ulio mlegevu, wa kivivu, na wa kizembe. Kila chembe ya nguvu yetu inapaswa kutumika, na fikira kali, tulivu, zenye kina zinapaswa kutumika. Hekima ya mjumbe ye yote wa kibinadamu haitoshi katika kupanga mipango na kubuni mbinu kwa wakati kama huu. Wekeni kila mpango mlio nao mbele zake Mungu kwa kufunga pamoja na kujinyenyekeza nafsi zenu mbele zake Bwana Yesu, na kuzikabidhi njia zenu kwa Bwana. Ahadi ya hakika ni hii, "Naye atayanyosha mapito yako [Atakuongoza katika njia zako - Mithali 3:5,6]. Yeye hana kikomo katika uwezo wake wa kusaidia. Mtakatifu wa Israeli, anayeliita jeshi lote la mbinguni kwa majina yake, na kuzishikilia nyota za mbinguni mahali pake, anawatunza ninyi kila mmoja peke yake....
Ningependa kwamba wote wapate kutambua uwezekano na mwelekeo uliopo kwa wale wote wanaomfanya Kristo kuwa utoshelevu wao na tegemeo lao. Uhai ule uliofichwa pamoja na Kristo katika Mungu daima unalo kimbilio; mtu huyo anaweza kusema, "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."
Jambo hili nawaachieni mikononi mwenu; kwa maana nimekuwa na wasiwasi na kusumbuka sana kwa ajili ya hatari zile zinazowashambulia wote walioko huko Battle Creek, ili wasije wakahama bila kuwa na tahadhari kubwa na [kwa kufanya hivyo] kumpa yule adui yetu faida kubwa. Jambo hilo halipaswi kuwa hivyo, maana kama tukienda kwa unyenyekevu na Mungu wetu, basi, tutakwenda salama. ----- Letter 45, 1893.